Macron, Le Pen wakashifiana hadharani
4 Mei 2017Kama ilivyokuwa imetazamiwa kabla, mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja kwenye televisheni ulikuwa wa piga-nikupige, kila mmoja akitumia maneno makali kadiri alivyoweza kuishusha hadhi ya mwengine mbele ya wapigakura wao, na pia akijidhihirisha alivyo na msimamo tafauti takribani kwenye kila jambo.
Ambapo Emmanuel Macron alijikita kwenye kunadi sera zake za uwazi na mageuzi ya soko, Le Pen alihamia zaidi kwenye msimamo wake wa uzalendo kwa Ufaransa. Tangu katika dakika ya mwanzo ya mdahalo huo, Le Pen alimpachika majina Macron akimuita "mgombea wa tabaka la wachache" na "kipenzi cha mfumo".
Majibu ya Macron dhidi ya tuhuma hizo, yalikuwa ni Le Pen, ambaye ni kizazi cha uongozi wa chama cha National Front, ndiye "mrithi wa mfumo ambao umeneemeka kutokana na majanga ya watu wa Ufaransa kwa miongo kadhaa", akiongeza kuwa Le Pen anacheza na hisia za khofu walizonazo watu ili kuvuna kura zao.
"Wewe hujali kuhusu nchi hii, huna mpango wowote nayo. Mpango wako ni kuwaambia Wafaransa mtu huyu ni mbaya, kuwachafua watu, kuongoza kampeni ya uongo na uzushi. Mpango wako ni kuwafanya watu waishi kwa khofu na uongo. Ndicho chakula chako. Ndicho chakula cha baba yako kwa miongo kadhaa, chakula cha Wafaransa wa mrengo mkali wa kulia na ndicho kilichokutengeneza wewe," alisema Macron.
Le Pen asema Ufaransa lazima itawaliwe na mwanamke
Kuhusu sera zao kuelekea bara la Ulaya, Le Pen alimtuhumu Macron kuwa myonge mbele ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, akidhihaki kwamba Ufaransa lazima itaongozwa tu na mwanamke, ama awe yeye, Le Pen, au Kansela Merkel.
"Ukweli ni kwamba ulikwenda kumuona Bi Merkel kumuomba baraka zake. Kwa sababu huwezi kufikiria kufanya jambo lolote bila ya ruhusa ya Bi Merkel. Ndio maana ulipoulizwa vipi utakabiliana na Merkel, ulisema hutokabiliana naye, bali utakuwa pamoja naye."
Wagombea wawili hao walionesha tafauti zao pia kuelekea uundikaji wa jamii ya Kifaransa, ambapo Macron alielezea Ufaransa ya mchanganyiko kama ilivyo, huku Le Pen akimtuhumu kuwa legelege sana dhidi ya Waislamu wenye siasa kali.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya Elabe na kuchapishwa muda mfupi baada ya mdhalo huo, ulionesha kuwa asilimia 63 ya watu walimuona Macron kuwa amewashawishi zaidi dhidi ya asilimia 34 za Le Pen.
Maoni ya jumla yanaonesha kuwa Macron atashinda kwa asilimia 59 dhidi ya 41 za Le Pen ikiwa uchaguzi utafanyika sasa, lakini midahalo kama hii ya lala salama huko nyuma imekuwa ikibadili muelekeo wa mambo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Daniel Gakuna