1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: Mataifa 26 yako tayari kupeleka Jeshi la Ukraine

5 Septemba 2025

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa mataifa 26 washirika wa Ukraine yameahidi kupeleka wanajeshi Ukraine kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama mara tu mapigano kati ya Ukraine na Urusi yatakapomalizika.

Ufaransa Paris 2025 | Mkutano na waandishi wa habari baada ya Muungano wa Mkutano wa Hiari na Volodymyr Zelensky na Emmanuel Macron
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Paris, Septemba 4, 2025.Picha: Ludovic Marin/AFP

Macron alitoa kauli hiyo baada ya mkutano uliofanyika jijini Paris wa kile kinachoitwa “Muungano wa Wenye Nia”, kundi la mataifa 35 yanayoiunga mkono Ukraine.

Alisema kuwa mataifa 26 kati ya hayoyamejitolea kupeleka wanajeshi nchini Ukraine au kudumisha uwepo wa kijeshi kwa njia ya ardhini, baharini au angani, ili kusaidia kuhakikisha usalama wa taifa hilo mara tu sitisho la mapigano au amani itakapofikiwa.

Mapema Alhamisi, Macron na viongozi wengine wa Ulaya walikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, pamoja na mjumbe wa Marekani kwa mazungumzo ya amani, Steve Witkoff, kujadili njia za kuhakikisha msaada wa kijeshi wa muda mrefu na kuendeleza uungwaji mkono wa Marekani kwa Ukraine baada ya mzozo kumalizika. Zelenskyy pia alifanya mkutano wa faragha na Witkoff.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na Rais Zelenskyy, Macron alisema jeshi hilo la kuhakikisha usalama “halina nia wala lengo la kuanzisha vita dhidi ya Urusi,” bali litakuwa na lengo la “kuzuia shambulio kubwa jipya na kuhusisha mataifa 26 moja kwa moja katika usalama wa kudumu wa Ukraine.”

Marekani yaonesha nia ya kushiriki ulinzi wa Ukraine

Macron alizungumzia pia ushiriki wa Marekani: "Walikuwa wazi sana wakati wa mkutano wetu na Washington. Na hili limerudiwa tena hapa. Hii pia ndiyo sababu waliunga mkono kazi ya wiki za hivi karibuni, msaada wao, na nia yao ya kushiriki katika dhamana za usalama. Kwa hiyo, hakuna kusitasita kuhusu suala hili." Ingawa maelezo ya kina kuhusu ushiriki wa Marekani bado hayajawekwa wazi, Macron na Zelenskyy walisema Washington imeonyesha nia ya kushiriki katika mpango huo.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakati mjini Paris.Picha: Ludovic Marin/AFP

Rais Zelenskyy alitoa shukrani zake kwa hatua hiyo na kusema "Tulikubaliana kwamba kutakuwa na uwepo wa vikosi. Bado siko tayari kuzungumzia idadi, ingawa, kwa kuwa mkweli, tayari tunaelewa takriban idadi ya wale waliokubali. Uwepo unaweza kuwa wa aina mbalimbali  angani, baharini, na ardhini."

Trump na NATO watoa kauli

Rais wa Marekani Donald Trump, kwa njia ya video, aliwahimiza viongozi wa Ulaya kuweka shinikizo la kiuchumi kwa China kwa sababu ya kuunga mkono uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Pia alisisitiza kuwa Ulaya inapaswa kusitisha ununuzi wa mafuta kutoka Urusi, ambayo yanafadhili vita.

Naye Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, alisema kuwa kunahitajika muungano mpana wa mataifa ili kuisaidia Ukraine kujilinda dhidi ya uchokozi wa Urusi, na pia kuimarisha uwezo wa Ulaya kuzuia hatua zaidi za kijeshi kutoka Moscow.

Mapigano yanaendelea Mashariki mwa Ukraine

Wakati hayo yakiendelea, mapigano kati ya Urusi na Ukraine bado yanaendelea. Usiku wa kuamkia leo, jeshi la Urusi lilishambulia kijiji cha Khotymlia katika mkoa wa Kharkiv kwa kutumia ndege zisizo na rubani (UAV), na kuua watu watatu wanaume wawili na mwanamke mmoja  huku wengine wawili wakijeruhiwa. Baadhi ya waathirika walikuwa wafanyakazi wa huduma ya ukarabati wa barabara.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW