Macron, Merkel wakubaliana Euro bilioni 500 kunusuru uchumi
19 Mei 2020Huku wakiweka kando tofauti za zamani na kutaka kuonyesha kuwa ushirikiano wa Ufaransa na Ujerumani ambao ndio kitovu cha Ulaya unabaki kuwa imara, Rais Emmanuel Macron na Kansela Angela Merkel wametangaza mpango huo wa kifedha usio wa kawaida baada ya mazungumzo kwa njia ya video.
Wakati uchumi wa Ulaya ukikumbwa na changamoto kubwa kabisa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Macron pia amekiri kuwa Umoja wa Ulaya haujafanikiwa katika namna ilivyoanza kulishughulikia janga la virusi vya corona na kwa hiyo unahitaji kushirikiana kwa karibu zaidi kuhusu suala la kiafya.
Taarifa ya viongozi hao wawili imesema kuwa fedha hizo zitakazotolewa kupitia ufadhili wa mikopo kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, zitapelekwa kwa sekta na maeneo ya umoja huo ambayo yameathirika pakubwa.
Merkel amesema kuwa wana uhakika kuwa sio haki tu bali pia ni muhimu kuzitoa fedha hizo, ambazo baadae zitarejeshwa pole pole kupitia bajeti kadhaa za siku za usoni za Ulaya. Macron ameongeza kuwa nchi zitakazonufaika na ufadhili huo hazitahitaji kurudisha fedha hizo, akisisitiza kuwa sio mikopo.
Soma Zaidi: Ulaya, Marekani kuingiza mabilioni ya dola kuziokowa chumi dhidi ya corona
Mpango huo wa mkopo unaashiria mabadiliko makubwa kwa Ujerumani, ambayo mpaka sasa imekuwa ikipinga miito ya Uhispania na Italia ya kile kilichoitwa "dhamana za corona” ambao ni mpango wa kukopa kwa pamoja kwenye masoko ya kifedha ili kutoa pesa ya kuufufua uchumi.
Ujerumani, Uholanzi na nchi nyingine tajiri ziliuona mpango huo wa dhamana za corona kuwa jaribio la upande wa kusini mwa Ulaya, wenye madeni kuidhulumu nidhamu ya kifedha ya upande wa kaskazini. Lakini Merkel amesema suala la mshikamano kwenye mgogoro huu wa kiafya lazima liwe la msingi.
Mpango huo wa Merkel na Macron hata hivyo hivi sasa unakabiliwa na kizingiti cha makubaliano magumu miongoni mwa wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya na hatimaye kura ya bunge la Ulaya ambalo limekuwa likitarajia kiasi kikubwa zaidi cha fedha. Mgawanyiko ndani ya umoja huo tayari umeanza kuonekana hasa baada ya Austria kusisitiza kwamba msaada wowote utatakiwa kuwa wa aina ya mkopo.
Rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen ambaye anatarajiwa kusaidia katika utekelezaji wake, ameyasifu mapendekezo ya mpango huo. Merkel amesema, ukubwa wa mzozo uliopo ulimaanisha kwamba kuna haja ya kuwepo kwa mshikamano kila wakati.
Macron amesema, ushirikiano thabiti wa Ulaya katika kukabiliana na mizozo ya kiafya ni lazima upewe kipaumbele, na kukiri kwamba umoja huo ulishindwa katika hatua za awali za kuushughulikia mzozo wa virusi vya corona. Aliongeza kuwa, hata hatua za baadhi ya mataifa kufunga mipaka bila ya kuwashirikisha majirani zao zilitoa picha mbaya kuhusu Ulaya zilizoonyesha ubinafsi wa mataifa hayo.
Mashirika: AFPE