1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Abbas wapanga kamati ya dola la Palestina

Amina Abubakar  dpa afp reuters
12 Novemba 2025

Ufaransa na mamlaka ya Palestina zimepanga kuunda kamati ya pamoja kushughulikia uimarishaji wa mpango wa kuundwa dola la Palestina huku Ufaransa ikiionya Israel dhidi ya kunyakuwa eneo la Ukingo wa Magharibi.

Emmanuel Macron na Mahmud Abbas
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Mamlaka wa Palestina Mahmud Abbas wamepanga kuunda kamati kwaajili ya mustakabali wa dola la Palestina.Picha: Christophe Ena/Pool/ABACA/picture alliance

Rais Macron amesema kamati itakayoundwa itashughulikia mambo yote ya kisheria, kikatiba, kuundwa kwa taasisi na kuratibu masuala ya uongozi. Aliyasema hayo wakati alipokutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas, mjini Paris kwa mazungumzo ya utekelezaji kamili wa makubaliano ya usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza. Macron amesema kamati hiyo pia inatarajiwa kuchangia pakubwa katika kuandaa katiba mpya.

Katika mkutano wao wa pamoja na waandishi habari mjini humo, Macron pia aliweka wazi kwamba Ufaransa isingelipenda kuwaona wanamgambo wa kipalestina Hamas, wakirejea uongozini Gaza.

"Kwa upande wa uongozi, Ufaransa haitaki kuona Hamas ikirudi na kuudhibiti Ukanda wa Gaza katika siku zijazo. Hili likitokea tutakuwa tumefeli kwa pamoja, ndiyo maana ni muhimu kufanyia kazi mchakato wa kuirejesha madarakani Mamlaka ya Palestina Gaza, na kuiondoa Hamas katika jukumu lolote la utawala wa eneo hilo, na kuipokonya silaha pamoja na kulisambaratisha kabisa kundi hilo."

Kwa upande wake Mahmud Abbas, ameunga mkono kikamilifu kuundwa kwa kamati hiyo ya pamoja akirejelea wito wake kwamba, taasisi za Gaza zinapaswa kudumisha uhusiano wake na mamlaka ya Palestina huku akisema anajitolea kusimamia uchaguzi wa rais Palestina baada ya vita kumalizika.

Haijawa wazi iwapo mamlaka ya Palestina itaidhibiti Gaza

Lakini suala la Mamlaka hiyo kuchukua udhibiti wa Gaza bado ni kitendawili. Hivi karibuni waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwa sasa haijawa wazi iwapo mamlaka hiyo ya palestina itakuwa na jukumu lolote katika hatma ya Ukanda wa Gaza.

Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud AbbasPicha: Fred Dugit/dpa/MAXPPP/picture alliance

Israel nayo siku zote imekuwa ikilipinga hilo huku kundi la wanamgambo wa Hamas, ambalo limekuwa likiuoongoza Ukanda huo tangu mwaka 2007 likipinga malaka hiyo kuchukua udhibiti wa Gaza.

Kwengineko kuhusiana na hali ilivyo katika Ukingo wa Magharibi, Macron alikosoa mashambulizi yanayofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya jamii ya wapalestina na kusisitiza kuwa mipango yoyote ya kulinyakuwa eneo hilo aidha kihalali au kiharamu inachora mstari mwekundu na kulazimisha majibu ya haraka kutoka Ulaya.

Kando na hayo Israel imesema imefungua kivuko muhimu kuingia Kaskazini mwa Gaza kwaajili ya kuruhusu misaada ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa kuingia huko. Msemaji wa mamlaka ya Israel inayosimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina, COGAT amesema kivuko hicho kitabakia wazi daima. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW