1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Merkel wakutana

Sekione Kitojo
19 Aprili 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewasili  mjini Berlin kwa mazungumzo na  kansela Angela Merkel yenye lengo la kupata  kuungwa mkono na kansela wa Ujerumani katika mipango yake ya mageuzi katika Umoja wa Ulaya, EU.

Berlin PK Merkel und Präsident Emmanuel Macron
Emmanuel Macron (kushoto) na Angela Merkel (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

 Kansela wa Ujerumani  amesema kwamba  licha  ya  kuwapo kwa tofauti  baina  ya  nchi yake  na  Ufaransa  katika  maeneo  machache ya pendekezo la  maguezi ya  EU, pande  hizo  mbili zitaweza kufanya kazi  kupata  muafaka  ifikapo  katikati  ya  mwaka huu.

Angela Merkel (kushoto) akisalimiana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron(kulia)Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

"Tunahitaji  kuwa  na mjadala  wa  wazi  na  hatimaye kupata  uwezekano  wa  kupata muafaka", Merkel amesema  mjini  Berlin leo wakati  wa  ziara  ya  rais  wa Ufaransa  Emmanuel Macron.  Ni  muhimu  kujibu  maswali muhimu  ya  wananchi  wa  Ulaya  kuhusiana  na changamoto za  dunia, alisema  wakati  akijadili mapendekezo  ya  Macron  kwa  ajili  ya  mageuzi  katika Umoja  wa  Ulaya.

Merkel  amesema  Ulaya  inaweza  tu  kutatua  matatizo yake  kwa  pamoja, amedokeza  kuhusu  sera  ya  uhamiaji ya  Umoja  huo, mtazamo  wa  pamoja  katika  sera  za mambo  ya  kigeni na  kuendeleza  zaidi uchumi  wa  eneo la  sarafu  ya  euro pamoja  na  umoja  wa  sarafu  kama maeneo  ambayo yeye  pamoja  na  Macron  bado hawajakubaliana.

Kansela  wa  Ujerumani  ana  imani  kwamba  Umoja  wa Ulaya  utafanikiwa kupata  matokeo mazuri  katika  maeneo mkubwa  ya  mageuzi, amesema  hayo  kabla  ya mazungumzo  na  rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron leo, akielezea  matumaini  juu  ya  kukamilisha  umoja  wa benki.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/V. Kessler

Mshikamano katika  kanda ya euro

Rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron alisema  kwamba mataifa  wanachama  wa  Umoja  wa  sarafu  ya  euro yanapaswa  kuongeza utaratibu  wa  mshikamano  kama vile umoja  wa  benki katika  mfumo  uliopo  hivi  sasa kwa lengo  la  kuimarisha  ushindani  iwapo  mataifa  hayo yatataka  kundi  hilo  la  mataifa  kuneemeka.

Kabla  ya kuanza  mazungumzo  yao, viongozi hao walisema watawasilisha  msimamo  wa  pamoja  mwezi Juni katika  mkutano  wa  viongozi  wa  Umoja  wa  Ulaya kuhusiana  na  mageuzi ya  kanda  ya  euro  yenye wanachama 19, ambapo Merkel  alisema  wamekubaliana lakini  bado hakuna  uhakika  wa  kutosha  kwamba hakutakuwa  na  mzozo.

"Nimefurahi  kwamba  Emmanuel Macron  amekubali mwaliko  wangu. Kwa sababu  huu  ni  mradi  wa  Ulaya na ni  mradi  ambao  tunataka  kuonesha  kwamba  sisi  ni sehemu  ya  dunia  na  tunataka  kufanya  mageuzi  na kuupa  sura utandawazi. Na  hiki  ni  kitu  ambacho kinatuunganisha  Ufaransa  na  Ujerumani."

Watu wa Ulaya wanatakiwa kuwa na mshikamano zaidiPicha: DW/L. Louis

Mkutano  wa  viongozi  hao  wawili  unafanyika  katika mazingira  ya  manung'uniko  ya  wabunge  wa  kundi  la vyama  vya  kihadihina  vinavyoongozwa na  Merkel , ambao  wanashaka  kwamba  wito  wa  Macron  wa mshikamano  zaidi   katika  kanda  ya  euro  unaweza kushuhudia  fedha  za  walipa  kodi  wa  Ujerumani zikitumika  kugharamia  mataifa  wanachama  wenye matatizo.

Mtazamo  wa Macron ni  pamoja  na  kubadilisha  mfuko uliopo  hivi  sasa  barani  Ulaya  wa  uokozi  wa  uchumi kuwa  kama  mfuko wa  fedha  wa  Ulaya EMF , na  kuwa kama kizuwizi  katika  mizozo  wa  hapo  baadaye  ya kifedha  katika  mataifa  hayo, ambayo karibu yaparaganyike  wakati  wa  mzozo  wa  madeni  mwaka 2009.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / dpae

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW