1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Putin kutafuta suluhisho la mzozo wa Ukraine

28 Januari 2022

Huku mzozo kati ya Ukraine na Urusi ukiendelea kutokota, rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kufanya mazungumzo kwa njia ya simu Ijumaa kuhusu suala hilo.

Kombobild Putin, Selenskyj & Biden
Picha: AFP

Mazungumzo hayo yanajiri baada ya mengine Alhamisi kati ya rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambapo Biden alimuahidi uungwaji mkono katika kukabiliana na Urusi. 

Katika mazungumzo ya Biden na Zelensky, Biden alikariri utayari wa Marekani pamoja na washirika wake kutoa jibu kamilifu ikiwa Urusi itaivamia Ukraine.

Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi

Hayo ni kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya Biden White House, iliyoeleza pia kwamba Biden alisema Marekani inazingatia misaada zaidi ya kiuchumi kwa Ukraine lakini bila kutoa maelezo zaidi.

Kwa upande wake, Zelensky aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba walikuwa na mazungumzo mazuri ya simu na Biden, na kwamba walijadili juhudi za kidiplomasia kuondoa wasiwasi uliopo, na wamekubaliana kwa hatua za pamoja katika siku zijazo.

Wajumbe wa Ukraine na Urusi wakutana Paris

Juhudi zaidi za kidiplomasia zahimizwa

Zelensky asema wamekubaliana na Biden kuhusu hatua za pamoja katika siku zijazo.Picha: Ukrainian Presidential Press/AP/picture alliance

Biden amekuwa akiongoza juhudi za kutafuta mshikamano wa nchi za magharibi dhidi ya shinikizo za jeshi la Urusi kwa Ukraine, hatua ambayo imeighadhabisha Urusi.

Urusi imewarundika zaidi ya wanajeshi wake 100, 000 karibu na mpaka wake na Ukraine. Nchi za magharibi zinahofia huenda Urusi inataka kuivamia Ukraine. Madai ambayo Urusi imekanusha.

Biden atishia kumwekea Putin vikwazo binafsi

Wito wa kupatikana suluhisho la amani na kuepusha vita umekuwa ukitolewa na wakuu mbalimbali ulimwenguni mfano Waziri Makuu wa Slovakia Eduard Heger.

"Lengo letu ni kuondoa wasiwasi na kushiriki mazungumzo. Na tunapozungumzia baadhi ya madhara, tunafanya hivyo ili yasitokee. Kuhakikisha kuna suluhisho la amani dhidi ya mzozo na taharuki iliyoko,” amesema Heger.

Mazungumzo ya Macron na Putin yatarajiwa kutoa suluhisho 

Macron anatizama mazungumzo kama nafasi ya kujua kwa yakini msimamo wa pande husika kuhusu hali ya sasa.Picha: Bertrand Guay/AFP/Getty Images

Kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kusuluhisha mgogoro huo na kuondoa hofu kwamba Urusi inapanga kuivamia Ukraine, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wanatarajiwa kuzungumza Ijumaa kwa njia ya simu.

Macron anatizama mazungumzo kama nafasi ya kujua kwa yakini msimamo wa pande husika kuhusu hali ya sasa. Anatumai Putin atatoa maelezo kuhusu baadhi ya masuala.

Marekani yawaweka wanajeshi 8,500 tayari, mzozo wa Ukraine

Duru katika ikulu ya Macron zimesema rais huyo anataka kusisitiza kwa mara nyingine kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine utakuwa na madhara makubwa.

Mkuu wa kundi la walioshinda tuzo ya amani ya Nobel Beatrice Fihn ambaye pia anaongoza kampeni ya kuachana na matumizi ya silaha za nyuklia, ametahadharisha kwamba mzozo unaohusisha nchi zenye silaha za nyuklia ni hatari sana.

Fihn amesisitiza haja ya kumaliza mvutano kwa dharura, akitaja zana za nyuklia katika mpaka wa Urusi lakini pia kwingineko Ulaya,  zinaweza kutumika endapo machafuko yatageuka vita.

Mrundiko wa wanajeshi wa Urusi katika mpaka wake na Ukraine umezusha hofu ya kwamba huenda Urusi inataka kuivamia Ukraine.Picha: Alexei Ivanov/AP/picture alliance

Uingereza yatahadharisha kuhusu udukuzi kutoka Urusi

Katika tukio jingine, Uingereza imezitahadharisha biashara kubwakubwa kuchukua hatua za kuzuia uwezekano wa mashambulizi ya mitandao au udukuzi kutoka Urusi.

Wito huo wa tahadhari umetolewa na kituo cha usalama wa kitaifa kuhusu mitandao cha Uingereza.

Mkurugenzi wa operesheni wa kituo hicho Paul Chichester amesema wameweza kubaini matukio ya kutia mashaka ya kimtandao kutoka Urusi katika miaka ya hivi karibuni.

Mvutano kati ya Urusi na Ukraine ulianza mwaka 2014. Mkataba wa amani uliosimamiwa na Ufaransa na Ujerumani kusuluhisha utata bado umekwama.

(DPA,AFP,RTR)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW