1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mada tete zaanza kujadiliwa katika mkutano wa hali ya hewa mjini Copenhagen

Oumilkher Hamidou8 Desemba 2009

Kansela Angela Merkel amezitolea mwito China na India ziwajibike zaidi katika kupunguza moshi wa viwandani

Kiwingu cha moshi kimetanda mjini BeijingPicha: AP

Masuala ya kiufundi yanagubika majadiliano mnamo siku ya pili ya mkutano wa kimataifa kuhusu hali ya hewa mjini Copenhagen.Mkutano huo wa kimataifa umechangamka kutokana na tangazo la shirika la ulinzi wa mazingira la Marekani EPA kuhusu uwezekano wa kusawazisha viwango vya moshi unaotoka viwandani.

Wakikutana katika mji mkuu wa Danemark hadi december 18 ijayo ili kusaka makubaliano ya kimataifa kupambana na kuzidi hali ya ujoto duniani,wawakilishi kutoka mataifa 193 wamejigawa makundi ili kushughulikia ipasavyo masuala mfano kuhusu namna ya kupambana na mitindo ya kufyekwa misitu,namna ya kugharimia miradi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa au kubuni utaratibu wa kuchunguza kama ahadi zitakazotolewa na nchi tofauti zinatekelezwa.

Tangazo la shirika la Marekani la hifadhi ya mazingira EPA la kupunguza moshi wa viwandani,unaotajikana kua sababu ya kuzidi hali ya ujoto duniani,na pia kua kitisho kwa afya ya binaadam,limepokelewa kwa furaha na wajumbe mkutanoni mjini Copenhagen.

"Litachangia kuwahakikishia wajumbe na wachunguzi wa nchi nyengine kwamba Marekani imepania kutumia njia zote zilizoko" amesema hayo David Doniger wa shirika lisilomilikiwa na serikali la "hifadhi ya raslimali ya taifa "la Marekani.

Shirika la walinzi wa mazingira Green Peace limelitaja tangazo la shirika la EPA kua ni "kichocheo muhimu" kwa mkutano wa Copenhagen.

Majadiliano kuhusu kupunguzwa moshi wa Carbon Diaoxide yanapamba moto na yanaendelea kwa siri katika kumbi mbali mbali za jengo la mkutano Bella Center wanakomiminika kila siku watu 15 elfu ,elfu tatu na mia tano kati yao wakiwa ni waandishi habari.

Kansela Angela Merkel akichambua hatari za kuzidi hali ya ujoto dunianiPicha: AP

Mjini Berlin,kansela Angela Merkel ambae sawa na rais Barack Obama wa Marekani na viongozi wengine kadhaa wa dunia,anapanga kushiriki katika awamu ya mwisho ya mkutano wa kilele wa hali ya hewa amezitolea mwito hii leo China na India zijitahidi zaidi katika suala la kupunguza moshi wa viwandani ili makubaliano yaweze kupatikana mjini Copenhagen.

Waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani Norbert Röttgen anaamini hata hivyo makubaliano yanaweza kufikiwa:Akihojiwa na kituo cha kwanza cha televisheni cha humu nchini ARD,bwana Norbert Röttgen amesema:

"La,hakuna njia ya kushindwa,na haistahiki kutokea kwasababu hatutomudu jambo hilo.Ni suala la kimsingi hili kuhusu mustakbal wa sayari yetu.Lakini si wote wamekubali kuitambua hali hiyo.Siku chache kabla China na India-zimeonyesha kusita sita.Lakini ndio maana tunaketi pamoja kujadiliana.Na tunaamini tutafanikiwa."

Mijadala moto moto kuhusu masuala ya kiufundi itaendelea kwa siku mbili tatu zijazo kabla ya mkutano wa mawaziri wa mazingira kuanza mwishoni mwa wiki hii.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir (afp/reuters)

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW