1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwendesha mashtaka ateuliwa kuchunguza madai

Abdu Said Mtullya25 Agosti 2009

Maafisa wa CIA wanadaiwa kutenda ukatili dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi.

Mtuhumiwa wakati akiteswa na maafisa wa CIA.Picha: picture alliance / dpa

Mwanasheria mkuu wa Marekani amemteua mwendesha mashtaka maalumu kuchunguza madai yaliyotolewa dhidi ya shirika la ujasusi CIA juu ya kuteswa kwa watuhumiwa wa ugaidi.

Kuteuliwa kwa mwendesha mashtaka huyo John Durham kumefuatia ripoti iliyochapishwa juu ya madai yanayowakabili maafisa wa CIA wanaodaiwa kutumia njia za kikaliti wakati wa kuwaisili watuhumiwa.

Kwa mujibu wa madai hayo maafisa hao waliwatisha mahabusi kwa silaha na kekee. Maafisa hao pia walimithilisha kuwanyonga watuhumiwa.

Ripoti hiyo pia inasema kwamba watoto wa watuhumiwa walitishiwa kuuawa na mama zao kubakwa.Licha ya madai hayo mwanasheria mkuu wa Marekani EricHolder amesema, hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya shirika la CIA inayoweza kuhatarisha usalama wa wamarekani.Hatahivyo mwanasheria mkuu huyo amesema , kulinda maslahi ya usalama wa taifa hakuna maana ya kuunga mkono njia za kikatili zilozotumiwa na maafisa wa CIA katika kuwahoji mahabusi wakati wa utawala wa rais G.Bush.

Ripoti juu ya madai ya ukatili uliotendwa na CIA ilitayarishwa mnamo mwaka 2004, lakini ripoti hiyo ilikuwa imechujwa kwa kiwango kikubwa.

Lakini hakimu aliamrisha kuchapishwa kwa ripoti yote baada ya jumuiya ya watetea haki za raia kuwasilisha mashtaka.

Rais Barack Obama sasa ameidhinisha jopo maalumu litakalowahoji watuhumiwa wa ugaidi. Wanajopo hao watatoka nje ya shirika la CIA.

Utawala wa Obama umesema kuanzia sasa uchunguzi wa watuhumiwa utafanyika kwa kufuata maagizo na taratibu zitakazowekwa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa jana, maafisa wa shirikka la CIA walitishia kuwaua watoto wa mtuhumiwa, Khalid Sheikh Mohammed ikiwa mashambulio zaidi ya kigaidi yangelifanyika. Pia walitishia kumbaka mama yake mbele yake ili kumdhalilisha.

Khalid Sheikh Mohammed anatuhumiwa kuwa mtu alieongoza mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika nchini Marekani tarehe 11 mwezi septemba mwaka 2001.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, palikuwa na mikasa kadhaa ambapo wafungwa nchini Irak au Afghanistan waliteswa na maafisa wa shirika la CIA.

Rais Obama amesema shirika la CIA halitakuwa tena linadhibiti masuala ya kuwahoji watuhumiwa.

Hatahivyo licha ya tuhuma hizo nzito rais Obama amesema anakusudia kusonga mbele badala ya kurudi nyuma. Msemaji wa Ikulu ameeleza kuwa rais Obama haoni haja yoyote ya kuwafuatilia wahusika waliokuwamo katika utawala wa rais G. Bush.

Mwandishi/Sina Ralph.

Imetasfiriwa na / Mtullya Abdu.

Mhariri/Abdul-Rahman.