1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madai ya ubakaji dhidi ya TB Joshua yawatikisa Wanjilisti

12 Januari 2024

Mwinjilisti wa televisheni wa Nigeria marehemu TB Joshua anatuhumiwa kufanya unyanyasaji mkubwa wa kingono. Madai haya yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya kanisa la kiinjili barani Afrika.

Nigeria  TB Joshua Mchungaji
Marehemu mchungaji TB Joshua anatuhumiwa kubaka dazeni kadhaa za wafausi wake.Picha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP via Getty Images

"Vyovyote itakavyokuwa, amekufa na kuondoka," Nkechi Anthony, mkazi wa Lagos na mshiriki wa kanisa la TB Joshua, aliiambia DW. "Kwa nini [tuhuma] hizo zote baada ya kifo chake?"

"Kwa mtazamo wangu, ushahidi na nyaraka zozote hazina msingi na hazina maana," alisema. Anthony ambaye ni Mkristo mwenye utashi, alikuwa akijibu ripoti ya uchunguzi wa shirika la utangazaji la BBC unaotaja waathirika wengi na vyanzo vinavyosimulia namna mwinjilisti mashuhuri wa televisheni nchini Nigeria hayati TB Joshua alivyowadhalilisha na kuwanyanyasa kingo wafausi wake.

TB Joushua alianzisha Kanisa la Sinagogi la Mataifa Yote - Synagogue Church Of All Nations (SCOAN) mjini LAgos, Nigeria, mnamo mwaka 1987.

"Maeneo zilikohifadhiwa kwa muda mrefu yalikuwa na usiri kiasi gani kiasi gani na hakuna aliyeona mambo haya yote hadi alipokufa?" Anthony aliuliza, akiongeza kuwa ripoti ya BBC "yote ni usaliti na haitaathiri uinjilisti nchini Nigeria kwa sababu sote tunajua madai hayo hayana msingi."

Jerry Edet, mwanachama mwingine wa kanisa la SCOAN la TB Joshua, alitetea sifa ya mchungaji wake, akiiambia DW madai yote yalikuwa ni udhalilishaji tu.

"Usimhukumu mtu yeyote wakati wewe mwenyewe utahukumiwa," alisema Edet. "Nimezunguka kanisa la sinagogi, hata nimelala huko na sijui hadithi hizi zote zinatoka wapi. Kwangu, inaweza kuwa aina ya uhuni."

Nini huwashawishi watu kufuata imani zenye utata za kidini?

02:15

This browser does not support the video element.

Tuhuma mbaya kwa kanisa

Lakini Joseph Adeleke, mchungaji anayeishi Lagos, hakubaliani. "Madai hayo yataleta mambo ya kutisha juu ya chombo hicho cha kiinjili, hasa sisi katika huduma ya kinabii, ukombozi na miujiza," aliiambia DW. "Itasababisha vikwazo vya kutisha kwa kanisa."

"Haya ni madai mazito ya ubakaji na miujiza ya uwongo. Wengi wa waumini wetu huenda wakapoteza imani kwa wachungaji na kanisa," alisema Adeleke na kuongeza kuwa kumekuwepo na tuhuma kama hizo dhidi ya baadhi ya wachungaji siku za nyuma. "Hii [madai ya ubakaji na mateso] ni kama kuthibitisha kile ambacho watu wamekuwa wakikisikia hapo awali."

Soma pia: Boko Haram wachinja 56 Nigeria

Maoni ya Adeleke yalishirikiwa hadi Afrika Kusini, ambapo TB Joshua alikuwa na ufuasi mkubwa. "Suala la wahubiri kushutumiwa kwa uhalifu huu wote ni mtindo," alisema Freeman Bhengu, Mratibu wa Kitaifa wa United Patriotic Front, asasi ya kiraia.

"Ni jambo ambalo limeenea katika Afrika, hasa Afrika Kusini, ambapo tumekuwa na wahubiri wanaobaka," Bhengu aliiambia DW.

"Tumekuwa na wahubiri wanaowafufua watu kwa uwongo, wahubiri wanaolaghai waumini wao kuwapa pesa. Tuhuma hizo zinasema kitu kuhusu sisi Waafrika Kusini. Zinasema kitu kuhusu sisi Waafrika. Bado ni wadhaifu kiakili. Bado tunalaghaiwa na manabii wa uongo kuhusu pesa rahisi, maisha rahisi, kila kitu cha haraka na kuridhika mara moja."

Kwa mujibu wa ripoti za ndani, Kanisa la SCOAN linapinga madai yote yaliotolewa dhidi ya TB Joshua katika filamu fupi ya BBC.

Mwanzo na utata wa TB Joshua

Temitope Balogun Joshua, maarufu kama TB Joshua na anaetajwa na wafuasi kama 'Mtume', alizaliwa Juni 12, 1963, huko Arigidi-Akoko, Jimbo la Ondo, kusini-magharibi mwa Nigeria.

Hadi kifo chake mwaka 2021, TB Joshua alikuwa amegeuka mwinjilisti mashuhuri wa televisheni.Picha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP via Getty Images

Alianza huduma yake ya kanisa mwishoni mwa miaka ya 1980 baada ya kudai wito wa kimungu akiwa na umri mdogo. Baada ya kuanzisha SCOAN mnamo 1987, alipata umaarufu haraka nchini Nigeria na kimataifa.

Kaisa la TB Joshua lilijikita kwenye tiba ya kiroho, uponyaji na unabii. Alikuja kujulikana pakubwa kwa injili yake ya televisheni na madai ya miujiza wakati wa mikutano hiyo. Wengi wa wafuasi wake na wahudhuriaji walidai kushuhudia uponyaji wa kimuujiza kupitia sala.

Huduma ya TB Joshua haikuwa bila utata. Wakosoaji waliibua wasiwasi juu ya ukweli wa miujiza na uponyaji, huku wengine wakimshutumu kwa kuwanyonya watu walio hatarini. Jarida la Forbes liliwahi kumwita "mchungaji wa Nigeria mwenye utata zaidi."

Soma pia:Madhehebu ya pentecosta Lagos,Nigeria 

Kwa Mabel Ndlovu, Mkristo wa Afrika Kusini, waumini wengi katika imani ya Kikristo wanahitaji kurudi kwenye kanuni za Biblia. "Ndani ya imani ya Kikristo kiwango ni kuwa kama Yesu na hiyo ni kufuata kile ambacho Biblia inatuongoza kufanya," Ndlovu aliiambia DW.

"Mambo haya mengi ambayo tunawaona [baadhi ya wahubiri] wakishutumiwa, hakuna hata moja kati ya hayo linalowakilisha imani ya Kikristo. Hakuna hata moja kati ya hayo linalowakilisha kile ambacho Kristo alifanya."

Ndlovu aliongeza kuwa watu wanapoamua kuwafuata viongozi fulani wa kidini, inasema, "tunakuamini wewe kama kiongozi ili utuwezeshe na ututie nguvu katika kutembea pia katika safari hii ya kutaka kuwa kama Kristo, na tunatarajia. wewe kushikilia na kuishi kulingana na viwango vya kibiblia."

Chomboa cha habari cha Sahara Reporters Jumanne kiliandika kwenye X, zamani Twitter, kwamba jukwaa la TV la TB Joshua, Emmanuel TV linasitisha huduma zake kwenye vituo kadhaa vya satelaiti.

Mnamo Aprili 2021, YouTube ilisimamisha chaneli ya TB Joshua baada ya shirika la kutetea haki la Open Democracy lenye makao yake nchini Uingereza kuwasilisha malalamiko dhidi ya baadhi ya video za mhubiri huyo ambazo zilidaiwa kumuonyesha akiomba "kuponya" mashoga.

Hakuna mashtaka kwa kuporomoka kwa jengo

Zaidi ya hayo, SCOAN ilikabiliwa na changamoto za kisheria na uchunguzi wa udhibiti. Kwa mfano, mwaka 2014, moja ya majengo ya kanisa hilo yaliyokuwa yakihifadhi wageni wa kimataifa liliporomoka na kuwaua watu wasiopungua 116, wengi wao kutoka Afrika Kusini.

Baada ya mkasa huo, uchunguzi wa eneo hilo uligundua "kanisa la TB Joshua lilikuwa na hatia ya uzembe wa uhalifu." Lakini hakuna mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya mwinjilisti huyo mashuhuri.

Kanisa la TB Joshua SCOAN pia liliendeleza juhudi za kibinadamu. SCOAN ilihusika katika shughuli mbalimbali za hisani, ikiwa ni pamoja na kusaidia watu wasiojiweza, kutoa ufadhili wa masomo, na kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii.

Hakuna alieshtakiwa kufuatia kuporomoka kwa jengo la TB Joshua lililoua watu 116.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Mnamo Juni 5, 2021, TB Joshua alikufa ghafla akiwa na umri wa miaka 57. Kifo chake kilivutia rambirambi na salamu kutoka kwa wafuasi, viongozi wa kidini na watu mashuhuri wa kisiasa kote Nigeria na kwingineko.

Baada ya kifo chake, kulikuwa na mijadala kuhusu mustakabali wa SCOAN na jinsi ushawishi wake ungeendelea kuliunda kanisa na wafuasi wake. Mkewe Evelyn, ambaye TB Joshua alizaa naye watoto watatu, sasa ndiye kiongozi wa huduma na anaendelea na utume wa marehemu mumewe kwa msaada wa wanafunzi kadhaa.