Madai ya upelelezi yaTrump hayana msingi,anasema mkuu wa FBI
21 Machi 2017Tunaanzia Marekani ambako madai ya rais Donald Trump anaemtuhumu mtangulizi wake Barack Obama kunasa mawasiliano yake yamebishwa moja kwa moja na mkurugenzi mkuu wa shirika la upelelezi la FBI James Comey. Akihojiwa na tume ya upelelezi ya baraza la wawakilishi, James Comey amethibitisha pia kuhusu uchunguzi kuhusiana na madai ya Urusi kushawishi kwa njia moja au nyengine uchaguzi wa rais nchini humo. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika: "Pengine haikuwa ajabu kwa mkurugenzi mkuu wa shirika la upelelezi la Marekani FBI James Comey kujitokeza mbele ya tume ya shughuli za upelelezi ya baraza la wawakilishi la Marekani, lakini alichokisema kilikuwa na umuhimu mkubwa. Alichokisema ni sawa na pigo kwa rais Trump. Kwanza kwasababu anathibitisha pia kuhusu uchunguzi unaoendelea wa ushahidi wa visa vya udanganyifu wakati wa uchaguzi, kwa msaada wa Urusi. Suala kama Trump binafsi amehusika bado si dhahir. Pigo kubwa zaidi ni pale Comey alipoyataja kuwa "hayana msingi," madai ya Trump kwamba mawasiliano yake yalikuwa yakisikilizwa na mtangulizi wake Barack Obama."
Uingereza kuwasilisha maombi ya kujitoa katika Umoja wa ulaya March 29
May 25 inayokuja Umoja wa Ulaya unaandhimisha miaka 60 tangu ulipoundwa. Siku nne baadae waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anapanga kuwasilisha rasmi maombi ya kujitoa katika umoja huo kufuatia kura ya maoni ya Brexit. Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung " linaandika: "Uingereza inaupatia Umoja wa Ulaya muda mfupi wa kusherehekea miaka 60 baada ya kutiwa saini makubaliano ya Roma-baadae wanawasilisha madai yao ya kujitenga.Tukio hilo la aina pekee, la kuagana ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya Umoja wa Ulaya, litafuata mkondo wake. Litakuwa tukio la kuagana kwa vishindo. Uingereza imetiliana saini maelfu ya mikataba tangu ilipojiunga na Umoja wa Ulaya miaka 45 iliyopita. Kuifuta mikataba yote hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ni ndoto. Serikali ya Uingereza inataka kuharakisha na kwa namna hiyo kupunguza gharama.Theresa May yuko tayari kusabilia uwanachama wa nchi yake katika soko la pamoja ili kulifikia lengo hilo. Lakini suala hapa halihusu pekee kile wakitakacho na wasichokitaka waengereza. Umoja wa Ulaya ndio wa kuyafungua majadiliano hata kama ni machungu. Na kutilia maanani ratiba au hali ikoje, itakuwa sawa na kujiaibisha tu."
Kampeni kali za uchaguzi Ujerumani
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kampeni za uchaguzi zilizopamba moto humu nchini. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: "Angela Merkel anaweza kweli kupambana? Anataka kweli kutetea madaraka? Masuala hayo wameanza tayari kujiuliza wafuasi wa chama chake cha CDU. Katika siasa ya ndani daima Merkel amekuwa akidhihirisha ana kipaji, la sivyo asingeweza kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama hicho cha kihafidhina. Lakini suala hapa ni jee anaweza kweli kuteremka katika ringi ya kampeni kali za uchaguzi dhidi ya Martin Schulz?
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman