Madai ya wizi wa kura yazusha malumbano Nairobi
11 Agosti 2022Ni malumbano katika mojawapo ya kituo cha kuhesabia kura jijini Nairobi kufuatia tuhuma na madai ya kuwepo wizi wa kura. Rabsha zimetokea usiku wa kuamkia Alhamisi katika kituo cha Jamhuri kwenye eneo bunge la Starehe pale wafuasi wa wawaniaji wa kiti cha ubunge wa eneo hilo walipokabiliana kwa cheche za maneno huku kila upande ukiwalaumu wapinzani wao.
Makabiliano hayo yaliendelea kwa muda hadi pale maafisa wa polisi walipoingilia kati na kudhibiti hali hiyo. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya, polisi wamewatia mbaroni washukiwa wawili kuhusiana na zogo hilo.
Wakenya wanasubiri kwa hamu kubwa matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.
Kwingineko, hali ya taharuki ilitanda katika kituo kimoja cha kuhesabia kura katika eneo bunge la Mathare kufuatia kuenea kwa uvumi kuwa kumetokea wizi wa kura.
Jiji la Nairobi limeshuhudia ushindani mkali kati ya wagombea kutoka muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais, Dokta William Ruto na ule wa Azimio la Umoja unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.