1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari Tanzania watenganisha watoto mapacha walioungana

Babu Abdalla Florence Majani
31 Januari 2024

Hospitali ya Muhimbili imeandika historia kwa kufanya upasuaji wa kuwatenganisha mapacha waliokuwa wameungana sehemu ya tumbo na kifua kwa upasuaji wa kwanza kufanywa na madaktari wazawa wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Madaktari wazawa wa Tanzania katika hospitali ya Muhimbili wakifanya upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha waliokuwa wameungana sehemu ya tumbo na kifua.
Madaktari wazawa wa Tanzania katika hospitali ya Muhimbili wakifanya upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha waliokuwa wameungana sehemu ya tumbo na kifua. Picha: Florence Majani/DW

Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji na madaktari wa watoto jana walitumia takribani masaa sita kufanya upasuaji huo mkubwa wa kuwatenganisha watoto mapacha walioungana sehemu ya tumboni na kifuani.

Hii ni mara ya kwanza kwa madaktari wazawa kufanya upasuaji huo kwani upasuaji kama huu wa kutenganisha watoto mapacha walioungana ulikuwa ukifanywa na wazawa kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Julai 1 mwaka jana, Muhimbili ilifanya upasuaji mkubwa wa kutenganisha mapacha Neema na Rehema walioungana sehemu ya kifua, tumbo na ini, ambao hata hivyo watoto hao baadaye walifariki. 

Soma pia: Kenya: Upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi waongezeka

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dokta Rachel Mhaville amesema watoto hao kwa sasa wanaendelea vizuri akizungumzia hasa kilichowezesha upasuaji huo kufanyika kwa mafanikio.

"Lakini kikubwa zaidi tunaweza kusema kwamba, tumeweka uwekezaji mkubwa kwanza kwa kusomesha madaktari bingwa, kuwa madaktari bingwa bobezi lakini pili vifaa, vifaa tiba na vifaa vya uchunguzi, vitu ambavyo vimetuwezesha kujua, ni wapi tupo na wapi tunaenda na jinsi gani tutawahudumia hawa watoto," amesema Dokta Rachel Mhaville.

Madaktari bingwa wazawa wahusika na upasuaji huo

Madaktari wa Tanzania katika chumba cha upasuaji hospitali ya MuhimbiliPicha: Florence Majani/DW

Akizungumzia mchakato wa upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Victor Ngota, amesema kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto unahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo ulihusisha jopo la wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa upasuaji watoto, wataalamu wa ini, upasuaji rekebishi, wataalamu wa usingizi, wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wa radiolojia.

"Tuliwapokea watoto hawa tarehe 11 Machi 2023 hivyo tulianza chakato wa kuwahusisha wataalamu ambao wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha."

Soma pia: Hospitali ya taifa Tanzania yazindua huduma ya kujifukiza

Dk Mhaville amesema, upasuaji wa aina hii kufanywa na wazawa unaashiria hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta ya afya na hivyo kutoa mwanya zaidi wa kuokoa maisha ya watoto mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana.

DW imezungumza na mchambuzi wa masuala ya afya na jamii, Bibiye Msumi, ambaye ametoa maoni yake kuhusu mapinduzi haya katika sekta ya afya Tanzania, "Inatuondolea sasa zile ghasia, bughdha na gharama, ambazo ilibidi tutumie kwenda nje ya nchi."

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyoanza kazi mwaka 1956 kwa sasa ina vitengo kadhaa, kikiwemo Chuo Kikuu cha Tiba na Kituo cha Utafiti, na ndiyo hospitali kubwa kabisa hapa nchini Tanzania ambayo imekuwa ikitowa huduma kwa wagonjwa hata kutoka mataifa ya jirani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW