1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madaktari wanne Zanzibar wafutiwa leseni za kufanyia kazi

26 Mei 2023

Wizara ya Afya visiwani Zanzibar imewafutia leseni madaktari wake wanne waliobainika kuhusika na uzembe wa kutotoa huduma kwa wakati, uliosababisha kifo cha mwanamke mmoja na mtoto wake wakati wa kujifungua.

DW Thumbnails Women in Kyiv give birth in bomb shelters
Picha: Mathias Bölinger/DW

Tukio hili la aina yake linatajwa kuwa ishara ya mabadiliko kwenye mwenendo wa wafanyakazi wa sekta ya afya ambao mara kadhaa wametajwa kwa visa vya uzembe, ufidhuli na dharau kwa wagonjwa.

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari hapo jana, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, alisema wameamua kuchukuwa hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa akinamama wanaokwenda kujifungua na wananchi wanaotaka huduma hospitalini.

Naibu wazir huyo alisema kuwa kwa hatua hiyo, serikali inakusudia kutoa fundisho kwa madaktari na wahudumu wa afya na kuwarejesha kwenye miongozo na maadili na kazi zao ili kila mwananchi  anayekwenda kwenye vituo vya afya apate huduma sawa na kwa wakati.

Wiki mbili zilizopita, Bi Kidawa Haji Khamis alipoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kujifungua, kufuatia wahudumu kumpuuza alipohitaji msaada ya kupandishwa juu ya kitanda. Inaelezwa kuwa Bi Kidawa aliishiwa nguvu na kuanguka chini, jambo ambalo lilisababisha mauti yeke na mwanawe tumboni.

Takwimu za wizara ya afya zinaonesha akina mama 287 kati laki moja hufariki dunia hapa Zanzibar wakati wa kujifungua.

Idadi hiyo ni kubwa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa na serikali inasema inajitihadi kuchukuwa hatua mbalimbali za kuimarisha huduma ya afya ili kupunguza vifo hivyo.

Mwandishi: Salma Said/DW Zanzibar

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW