1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madeni makubwa ya Uganda yawatia raia tumbojoto

Lubega Emmanuel8 Januari 2019

Uganda inadaiwa kiasi cha asilimia 41 ya pato jumla la taifa. Deni la taifa la Uganda limeanza kuwatia wasiwasi Waganda wengi wakihofia kuwa hali hii itazidi kuzorotesha ukuaji wa uchumi wa nchi.

UGANDA Finanzminister Matia Kasaija (L)
Picha: Getty Images/AFP/I. Kasamani

Deni la taifa la Uganda limeanza kuwatia wasiwasi Waganda wengi wakihofia kuwa hali hii itazidi kuzorotesha ukuaji wa uchumi wa nchi. Kulingana na wizara ya fedha, Uganda inadaiwa kiasi cha asilimia 41 ya pato jumla la taifa na itaendelea kuchukua mikopo kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ili kubuni fursa za ajira na uwekezaji.

Lakini wadadisi wa masuala ya madeni na uchumi wa nchi wana mashaka kama taifa litakuwa na uwezo wa kukidhi mzigo huo mkubwa wa medeni unaongezeka kila kukicha. China ndiyo inaongoza katika kuidai Uganda kiasi kikubwa na kuna hofu kuwa huenda nchi hiyo itatwaa mali za Uganda ili kujilipa deni lake.

Mara kwa mara serikali ya Uganda husaini mikataba ya mikopo na mataifa na mashirika mbalimbali ya kigeni kwa ajili ya kile kinachotaja kuwa ujenzi wa miundombinu kuchapua maendeleo ya kiuchumi, kijamii na usalama wa nchi. Miongoni mwa hayo ni barabara na madaraja, mabwawa ya kuzalisha umeme na kadhalika. Serikali inasema kuwepo kwa miundombinu hii japo inatokana na mikopo, ni hatua muhimu katika kubuni nafasi za kazi pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni. 

Waziri amefafanua kuwa serikali inafahamu kuwa deni la nchi linazidi kuwa kubwa lakini hali hii haiepukiki ikiwa taifa linataka kuimarika kiuchumi katika siku za usoni. Lakini kwa mtazamo wa baadhi ya wananchi, mwenendo huu wa kukopa kila mara unazidi kuitumbukiza Uganda katika lindi la shida za kiuchumi ambazo tofauti na matarajio ya serikali, itakuwa kazi kubwa kujikwamua.

Rais Museveni ameliongota taifa la Uganda kwa zaidi ya miaka 30Picha: Imago/ITAR-TASS/A. Shcherba

Kwa sasa Uganda inabeba mzigo wa madeni ambao ni asilimia 41 ya pato jumla la taifa. Hofu na mashaka ni kwamba huenda nchi kama China inayoidai Uganda angalau asilimia 25 ya deni la nchi imeanza kutumia mbinu inazoacha mianya ya kutwaa mali za nchi kama ilivyokuwa kule Zambia. 

Lakini waziri wa fedha Matia Kasaija anakanusha vikali uwezekano wa hatua kama hii kuchukuliwa akisisitiza kuwa Uganda ina uwezo wa kuyalipa madeni yake kwa mujibu wa mikataba iliyosaini.

Mtaalamu wa masuala ya bajeti Julius Mukunda wa shirika la CSBAG ametahadharisha Waganda kuwa wasichangamkie kuongezeka kwa bajeti ya nchi ya mwaka ujao wa kifedha kwani hadi asilimia 40 ya fedhaa kwenye bajeti hiyo zitatumiwa kulipa madeni pamoja na riba.

Kile ambacho kimevutia Uganda pamoja na mataifa mengine ya Afrika kuchukua madeni hususan kutoka China ni kile kinachodaiwa kuwa masharti yake nafuu ikilinganishwa na mataifa na mashirika ya kimagharibi ambayo hutaka haki za binadamu kuzingatiwa, pamoja na utawala bora.

Lakini kwa mtazamo wa wadadisi wa kiuchumi, masharti ya China kutaka makampuni kutoka nchi hiyo tu kupewa kandarasi za miradi wanayofadhili pamoja na kuagizwa kwa vifaa kutoka nchi hiyo tu hata kwa njia ya mikopo ni dhana inayoikosesha nchi inayochukua mkopo fursa ya kukuza makampuni ya wazawa pamoja na kubinya uwezo wa kitaaluma wa watu wake.

Mwandishi: Lubega Emmanuel.

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW