Madhila ya wanawake wa Rohingya katika kambi za Bangladesh
5 Februari 2024Wakimbizi wapatao milioni moja wa jamii ya Rohingya wanaishi kwenye mabanda yaliyojengwa kwa mianzi na mifuko ya plastiki katika kambi ya Cox's Bazar, mojawapo ya kambi kumbwa kabisa kusini mwa Bangladesh.
Warohingya hao, ambao kwa dini yao ni Waislamu, walikimbia mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kikabila na kidini nchini Myanmar, taifa linalofuata dini ya Kibuddha, na ambalo limekuwa likiwakataa.
Kwenye miaka ya karibuni, hali ya usalama kwenye kambi za wakimbizi imekuwa ikizorota, ambapo mashambulizi ya kijinsia, utekaji nyara na mauaji yamekuwa matukio ya kila siku.
Kambi hizo zimejaa magenge ya kihalifu na pia makundi ya waasi wa Kirohingya. Wakaazi wa kambi hizo wamelalamikia pia udhalilishaji unaofanywa na vyombo vya usalama vya Bangladesh dhidi yao.
Wito wa UN: UN yatoa wito kuokolewa Warohingya 185 bahari ya Hindi
Mwanamke mmoja wa miaka 22 anayeishi kwenye kambi ya Balukhali ndani ya eneo la Cox's Bazaar alisema afisa mmoja kutoka Kikosi Maalum cha Polisi ya Bangladesh kilichotumwa kambini hapo, amekuwa akimfuatilia kwa miezi kadhaa sasa.
Anasema usiku wa tarehe 7 Januari, aliingia nyumbani mwao kwa kisingizio cha operesheni ya usalama na akajaribu kumbaka. Aliokolewa na majirani baada ya kupiga makelele ya kuomba msaada. Afisa huyo akiwa na wenzake wawili alikimbia baada ya wakimbizi kukusanyika wakijaribu kuwakamata.
Mume wa mwanamke huyo aliiambia DW kwamba wamekuwa wakitishiwa maisha yao tangu walipoandikisha maelezo ya tukio hilo kwa mkuu wa kambi hiyo ya wakimbizi.
"Tumeambiwa tuondoshe kesi yetu au wanasema watanikamata kwa kesi ya kubuni na kuniweka ndani.” Alisema mwanamme huyo.
Soma pia: Takriban Warohingya 170 wamewasili Indonesia
Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch linautaja mkasa huo kwenye ripoti yake iliyopewa jina: "Polisi wa Bangladesh wafanya udhalilishaji kwenye kambi za Warohigya.” Shirika hilo liliutaka uongozi wa Bangladesh kuchunguza madai hayo kwa kina na kwa uhuru na kuwapa ulinzi wakimbizi walioko kambini.”
Kamishna wa wakimbizi wa Bangladesh kwenye kambi ya Cox's Baraar, Mohamed Mizanur Rahman, alikiri mbele ya DW kwamba alijuwa kuhusu jaribio hilo la ubakaji kwenye gazeti, akisema amezitaka mamlaka kulichunguza.
Kamishna huyo aliongeza na hapa namnukuu: "Nimeliwasilisha suala hili kwa naibu mkuu wa polisi ili kulichunguza. Sijapata taarifa yoyote hadi sasa. Lakini hakuna aliyeleta malalamiko kwangu au mkuu wangu wa kambi. Kwa hivyo siwezi kusema mengi zaidi.” Mwisho wa kumnukuu.
Wakimbizi wengi waliozungumza na DW walisema ni shida kwao kupata msaada wa kisheria au kuandiisha malalamiko rasmi kwenye vituo vya polisi juu ya matukio ya ubakaji na mauaji yanayofanywa na jeshi hilo.
Abdul Ghafur, mkiizi ambaye kwa miaka 34 amekuwa akiishi kwenye kambi ya Kutupalong, aliiambia DW kwamba mwili wa binti yake mwenye umri wa miaka 17 ulikutwa karibu na hoteli moja asubuhi ya tarehe 2 Agosti 2022.
Abdul Ghafur aliongeza na hapa namnukuu: "Binti yangu alibakwa na kuuawa usiku uliotangulia. Kulikuwa na alama za kuteswa kwenye mwili wake. Kulikuwa na alama za kutafunwa kwenye mgongo wake, midomo yake ilichomwa kwa sigara, na kifua chake kilivunjika kabisa.” Mwisho wa kumnukuu.
Bofya hapa: Mkuu wa UN atoa wito wa kuwasaidia Warohingya
Baba huyo anawatuhumu maafisa wa polisi kuwa walimteka binti yake akiwa kwenye kiwanda cha nguo karibu na kambi hiyo, ambako alikuwa akifanya kazi ya kujitolea, kisha wakambaka na kumuua.
Hata hivyo, Abdul Ghafur hakuweza kuandikisha malalamiko polisi wala kufunguwa kesi mahakamani. Sababu ni kuwa wanahitaji ruhusa ya mkuu wa kambi ili waweze kwenda nje ya kambi, naye alikataliwa kwenda baada ya kuwataja maafisa wa polisi kuwa ndio watuhumiwa wake wakuu.
Mwanamke mwengine mwenye umri wa miaka 27 kwenye kambi hiyo, aliiambia DW kwamba maafisa wa polisi walijaribu kumbaka mwaka jana wakati akirejea nyumbani kutoka hospitalini nyakati za usiku.
Kwa maneno yake mwenyewe, walimchania nguo zake na kumtomasa kifuani huku wakijaribu kumbaka karibu kabisa na kizuizi cha polisi. Mama huyo wa Watoto watatu anasema alipelekwa kituo cha polisi ambako aliteswa hadi akapoteza fahamu. Kisha akakamatwa kwa mashitaka ya kubuni na kufungwa jela kwa miezi mitatu.
Watu 6 wauwawa katika makabiliano kwenye kambi ya wakimbizi Bangladesh
Anaongeza na hapa namnukuu: "Polisi wanamdhalilisha mwanamke yeyote wanayemuona mzuir kwenye kambi. Wanawatomasatomasa mashavu na vifua mitaani na wanafuata nyumbani usiku ili kuwabaka.” Mwisho wa kumnukuu.
Binti mwengine mwenye umri wa miaka 18 aliiambia DW kwamba maafisa wa polisi walimbaka kwenye kibanda chao kambini hapo miaka miwili iliyopita walikokwenda kwa kisingizio cha kumkamata kaka yake.
"Nilibakwa mara kadhaa. Nahisi siko salama hapa kambini. Naiomba serikali ya Bangladesh kutuhakikishia usalama wetu." Anasema.
Wakimbizi wote hawa wanasema hawakuweza kuandikisha malalamiko rasmi kituo cha polisi wala kufunguwa kesi mahakamani kusaka haki zao na kwamba kwenye matukio yote hayo, hakuna mtuhumiwa aliyeadhibiwa.