Maduro aapa kupambana na Marekani, Colombia
27 Machi 2020Masaa kadhaa baada ya Marekani kumfungulia mashitaka ya kuendesha biashara haramu ya madawa ya kulevya na kutangaza dau la dola milioni 15 kwa atakayemkamata na kumpeleka Washington, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameiita hatua hiyo kuwa ya kibaguzi na kuonya kuwa yuko tayari kupambana kwa njia yoyote ile endapo Marekani na Marekani zitajaribu kuivamia nchi yake.
Kauli hiyo ya Maduro aliyoitoa usiku wa kuamkia leo ilikuja ikiwa ni masaa machache baada ya Marekani kutangaza mashitaka kadhaa dhidi ya kiongozi huyo wa kisoshalisti na washirika wake kadhaa, ikiwatuhumu kuigeuza Venezuela kuwa genge la kihalifu linalotumikia walanguzi wa madawa ya kulevya na makundi ya kigaidi.
Katika moja ya mashitaka hayo, waendesha mashitaka mjini New York wanamtuhumu Maduro na mkuu wa bunge kutokea chama chake cha kisoshaliti, Diosdado Cabello, kwa kula njama na waasi wa Colombia pamoja na wanajeshi "kujaza madawa ya kulevya nchini Marekani” na kutumia biashara ya madawa hayo kama "silaha dhidi ya Marekani.”
Maduro, dereva wa zamani wa basi ambaye anajitambulisha kama alama ya wanasiasa wa mrengo wa kushoto katika Amerika ya Kusini, ameyaita mashitaka hayo ni ya kisiasa, akihoji kwamba yanapuuza dhima ya mshirika wa Marekani, Colombia, kama chanzo kikuu cha madawa ya cocaine duniani na pia dhima yake mwenyewe Maduro ya kuwezesha mazungumzo ya kutafuta amani kati ya serikali ya Colombia na waasi wa nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mzima.
'Trump, wewe ni ovyo kabisa'
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Maduro alisema, "Donald Trump, wewe ni mwanaadamu wa ovyo kabisa. Unayaendesha mahusiano ya kimataifa kama msanii wa kimafia wa New York na bosi wa makampuni ya udalali.”.
Kiongozi huyo, ambaye mwaka jana alikabiliwa na kushinda jaribio la mapinduzi linalosemekana kuchochewa na Marekani, aliapa kuchukuwa hatua zozote kujilinda, akitishia kuwa endapo wale aliowaita mabeberu na kibaraka wao Colombia watajaribu kumgusa hata unywele, basi atawaangamiza mara moja.
Mapema, mwendesha mashitaka mkuu wa Venezuela alianzisha uchunguzi dhidi ya kiongozi wa upinzani, Juan Guaido, akimtuhumu kwa jaribio la mapinduzi kwa kushirikiana na jenerali mstaafu wa jeshi, Cliver Alcala, ambaye baada ya kutajwa kwenye mashitaka ya Marekani, alisema alikuwa amekusanya rundo la silaha nchini Colombia kwa ajili ya uvamizi dhidi ya Venezuela. Maduro anaamini kuwa Jenerali Alcala alikula njama ya kumuua yeye na wenzake serikalini.
Mashitaka dhidi ya kiongozi wa nchi aliye madarakani si jambo la kawaida na hapana shaka yataongeza uhasama kati ya Washington na Caracas. Mashitaka yaliyofunguliwa na Marekani yanarudi nyuma hadi mwanzoni mwa mapinduzi yaliyoongozwa na mtangulizi wa Maduro, Hugo Chavez, mwaka 1999 na yanahusisha mataifa mengine kama Syria, Mexico, Honduras Iran.
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr, anadai kuwa njama hizo zilisaidia kuingizwa kwa tani 250 ndani ya Marekani kwa kila mwaka kutoka Amerika ya Kusini.
Vyanzo: ap, rtre