1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Maduro afikishwa katika Mahakama ya New York

5 Januari 2026

Kiongozi wa Venezuela aliyeondolewa madarakani Nicolás Maduro amefikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama nchini Marekani akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi na kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

New York I Aliyekuwa Kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro akifikishwa mahakamani
Kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Venezuela Nicolas Maduro akifikishwa mahakamani mjini New York chini ya ulinzi mkaliPicha: Kyle Mazza/Consolidated News Photos/picture alliance

Maduro na mkewe wamefikishwa mbele ya jaji Alvin Hellerstein wa Mahakama ya Shirikisho ya Manhattan mjini New York chini ya ulinzi mkali, hii ikiwa ni hatua muhimu ambayo huenda ikaanzisha mvutano mrefu wa kisheria wa kufahamu ikiwa Maduro na mkewe wanaweza kushtakiwa nchini Marekani.

Mawakili wa  Nicolas Maduro  wamesema watapinga kwanza uhalali wa kukamatwa kwake, wakisema mteja wao anayo kinga ya kushtakiwa kwa kuwa ni mkuu wa taifa huru la kigeni. Madai ambayo bila shaka yatatupiliwa mbali na Marekani ambayo haimtambui Maduro kama kiongozi halali wa Venezuela.

Maduro, mkewe, mwanawe na watu wengine watatu, wanatuhumiwa kwa kushirikiana na magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya wakirahisisha usafirishaji wa maelfu ya tani za kokeini nchini Marekani. Ikiwa watakutwa na hatia, wanaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha jela.

Hali ya wasiwasi yashuhudiwa kimataifa

Rais wa mpito Delcy Rodríguez aliyehudumu kama makamu wa rais tangu mwaka 2018 na aliyechukua nafasi ya mshirika wake Maduro, sasa ametangaza "kushirikiana" na utawala wa Trump katika kile kinachotazamwa kuwa  ni mabadiliko makubwa katika uhusiano kati ya Washington na Caracas.

Hata hivyo wachambuzi wanasema azma ya Marekani ya kutaka kuhodhi sekta ya mafuta ya Venezuela, itakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na hatua zitakazochukuliwa na  Urusi na China  ambazo hazitokubali kuona uwekezaji wao wa mabilioni ya dola katika sekta ya mafuta huko Venezuela ukipotea.

Watu wakiandamana nje ya Mahakama huko New York wakidai Maduro aachiwe huruPicha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine, ukosoaji wa kimataifa umeendelea kufuatia kitendo cha kutekwa kwa Maduro na makomandoo wa Marekani, huku baadhi ya mataifa yakishindwa kuwa na msimamo wa wazi juu ya tukio hilo.

Ujerumani kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Johann Wadephul ametoa wito wa kurejesha hali ya utulivu wa kisiasa huko Venezuela na kusisitiza kuwa linalopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni kutafuta namna ya kusonga mbele kwa kuzingatia sheria za kimataifa, demokrasia na kujitawala kwa watu wa Venezuela.

" Watu wa nchi hiyo wanaweza kujiamulia mustakabali wa nchi yao na wanapaswa kupewa fursa ya kufanya hivyo haraka iwezekanavyo kulingana na sheria na kanuni za kimataifa. Tutatoa mchango wetu katika mchakato huu mara tu utakapoanza, ” aliongeza waziri Wadephul.

Tukio la Marekani kumteka Maduro limezusha hali ya wasiwasi kwa mataifa mengine ambayo yamekuwa na msuguano na Trump. Rais wa  Colombia Gustavo Petro amesema hivi leo kuwa yuko tayari "kuchukua tena silaha" ili kuilinda nchi yake, baada ya Trump kusema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Petro anapaswa "kuwa makini" huku akimtaja rais huyo wa Colombia kuwa ni " mgonjwa wa akili anayezalisha kokeini na kuiuza nchini Marekani."

(Vyanzo: Mashirika)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW