1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduro akataa kuitisha uchaguzi wa rais

30 Januari 2019

Kiongozi huyo wa Venezuela amesema yuko tayari kwa mazungumzo na upinzani na kuitisha uchaguzi wa mapema wa bunge wakati ambapo mpinzani wake Guaido amechachamaa kuitisha maandamano zaidi

Venezuela Caracas Nicolas Maduro
Picha: Reuters/Miraflores Palace

Mapambano ya kuwania madaraka ya  kuidhibiti Venezuela yamepamba moto baada ya serikali hii leo kushinikiza uchunguzi ambao huenda ukasababisha kukamatwa kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa mpito nchini humo Juan Guaido ambaye wakati huohuo ameitisha upya maandamano mengine.

Mahakama ya juu kabisa ya Venezuela imepitisha vikwazo dhidi ya Guaido kusafiri nje ya nchi hiyo na akaunti zake kuzuiliwa. Hatua hii inaonekana pengine inalenga kulipitiza kisasi kutokana na vikwazo ilivyowekewa Venezuela na Marekani  katika biashara yake ya Mafuta.Vikwazo hivyo hapana shaka vinatarajiwa kuutikisa kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi hiyo mwanachama wa shirika la nchi zenye kuzalishwa kiwango kikubwa cha mafuta duniani OPEC,uchumi ambao tayari umeshaporomoka.

Picha: Getty Images/AFP/C. Ramirez

Guaido anatambuliwa kama rais na Marekani pamoja na nchi nyingi za Magharibi huku akionekana kuupa changamoto kubwa utawala wa miaka sita wa rais Nicolas Maduro. Rais Trump wa Marekani amesema serikali yake pia inamtambua mjumbe wa kidiplomasia kutoka upande wa upinzani wa Guaido katika ubalozi wa Venezuela nchini Marekani, Carlos Alfredo Vecchio.Mjumbe huyo baada ya kukutana na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence jumanne aliutolea mwito ulimwengu kusaidia kuikomboa Venezuela.

''Tuliweka wazi kwamba hivi vita sio kuhusu itikadi. Hivi ni vita kati ya demokrasia na udikteta. Hivi ni vita kati ya udikteta ambao kwa hali zote unaendeshwa na utawala wa Cuba dhidi ya ulimwengu ulio huru. Hatuwezi kushinda vita hivi peke yetu.Tuna majukumu makubwa kama wavenezuela lakini tunawaomba nyinyi ulimwengu ulio huru kutukomboa kwa namna fulani, Venezuela ambayo iko kwenye ukoloni wa utawala wa Cuba. Kwa hivyo tutaendelea kupambana mpaka tutakapoipata tena demokrasia yetu na ndio sababu tutaendelea kuomba msaada wa Kimataifa''

Picha: Getty Images/AFP/Y. Cortez

Kiongozi wa upinzani Guaido ameitisha maandamano zaidi leo Jumatano pamoja maandamano mengine mwishoni mwa wiki ili kuendelea kumshinikiza rais Maduro kupitia sauti za wananchi mitaani. Maduro ambaye anamtuhumu Guaido kuendesha jitihada zinazosimamiwa na Marekani za kutaka kumpindua madarakani bado anaungwa mkono na uongozi wa juu jeshini na hakuna dalili kwamba atasalimu amri labda mambo yabadilike.

Hii leo rais huyo amesema atakuwa tayari kuitisha  uchaguzi wa bunge wa mapema lakini amekataa katakata uchaguzi mpya wa rais, na amesisitiza  anataka mazungumzo na upinzani unaoungwa mkono na Marekani na ikiwezekana paweko na nchi nyingine itakayosimamia mazungumzo hayo. Msimamo huo mpya wa Maduro umetangazwa na shirika la habari la Urusi RIA ambalo pia limeripoti kwamba Maduro amesema rais Vladmir Putin wa Urusi ameahidi kumpa msaada zaidi wa kiuchumi na kijeshi. Kwa upande mwingine lakini Juan Guaido ameutaka Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo zaidi kama ilivyofanya Marekani dhidi ya serikali ya rais Maduro baada ya kuhojiwa na gazeti la Ujerumani la Bild.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW