1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduro ashinda uchaguzi Venezuela

Daniel Gakuba
21 Mei 2018

Tume ya uchaguzi wa Venezuela imemtangaza Rais Nicolas Maduro kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Jumapili, ambao ulisusiwa na upinzani. Kulingana na tume hiyo, Maduro amepata zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa.

Venezuela Wahlen - Nicolas Maduro
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Cubillos

Ni matokeo ambayo hayakuwashangaza watu kwa sababu chama kikuu cha upinzani kiliususia uchaguzi huo, na kisha, wapinzani wawili wakuu wakazuiwa kugombea. Na siyo hayo tu, kwa sababu hata tume ya uchaguzi inaripotiwa kuendeshwa na washirika wa karibu wa Rais Nicolas Maduro.

Tume hiyo imesema Maduro aliungwa mkono kwa kura milioni 5.8 ambazo ni sawa na asilimia 67.7, akifuatiwa kwa mbali na Henri Falcon, gavana wa zamani wa jimbo ambaye alikihama chama tawala cha kisoshalisti mwaka 2010, aliyepata kura milioni 1.8, sawa na asilimia 21.2. Katika nafasi ya tatu yuko mhubiri wa kievanjelisti Javier Bertucci, aliyeambulia asilimia 11 ya kura zilizopigwa.

Akiuhutubia umati wa wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi, Rais Maduro alisema wapinzani wake walijidanganya sana kuhusu uwezo wake na kuwashukuru waliomchagua.

Tume ya uchaguzi ilielezwa kuwa mshirika wa MaduroPicha: Reuters/M. Bello

''Asante sana kwa kushinda manyanyaso mengi na kuupuza uongo mwingi. Asante kwa kushiriki katika mapambano mengi na asante kwa kunifanya rais wa Jamhuri ya Kibolivari ya Venezuela, kwa muhula wa 2019 hadi 2025. Asante watu wapendwa wa Venezuela''. Alisema Maduro.

Uitikiaji wa chini mno

Uchaguzi huo wa jana Jumapili uliitikiwa kwa kiwango cha chini, ambacho tume ya uchaguzi imesema kilikuwa asilimia 46.1, lakini wapinzani wakiweka makadirio yao kuwa asilimia chini ya 30. Chanzo kutoka tume ya uchaguzi kimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa asilimia 32.3 ya watu wenye sifa za kupiga kura ndio waliokuwa wamefika vituoni hadi saa kumi na mbili jioni.

Henri Falcon aliyekuja katika nafasi ya piliPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Llano

Wakati Rais Maduro na kambi yake wakisherehekea, wapinzani wanalalamika. Henri Falcon aliyeshika katika nafasi ya pili amesema hakuna shaka lolote kwamba uchaguzi huo ulikosa sifa za kuwa wenye uwazi na wa kuaminika.

Alisema, ''Katika hali kama hii, ni wajibu wetu kulaani kwa sababu makubaliano yaliyosainiwa hayakuheshimiwa, na kwa hiyo, hatuutambui mchakato huu wa uchaguzi kuwa halali. Kwetu na kama hakuna uchaguzi uliofanyika. Uchaguzi mpya unahitajika kuandaliwa nchini Venezuela.''

Mkakati uliokwenda vibaya

Maduro alikuwa amemkaribisha Falcon kusimama dhidi yake, hali ambayo iliufanya uchaguzi huo uliosusia na wapinzani wengine kuwa na thamani. Hatua ya Falcon kuulani mara moja, ni pigo kwa mkakati wa serikali ya Maduro. Falcon alisema wapiga kura wengi masikini walitakiwa kuzipiga picha kadi zao za kupiga kura katika vituo mahema ya wafuasi wa Maduro waliokuwa wamepiga kambi karibu na vituo vya kupigia kura, kuthibitisha kwamba wamemchagua Maduro ili baadaye wapewe zawadi, Falcon amesema hiyo haikuwa tofauti na kuziuza kura zao.

Katika ishara kwamba muhula huu mpya wa Rais Maduro utakabiliwa na changamoto kali, utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump umesema hautautambua uchaguzi huo, na unapanga kuiwekea vikwazo sekta ya mafuta ya nchi hiyo. Kitisho hicho cha Marekani ni kama msumari mwingine kwenye jeneza la uchumi wa Venezuela ambao tayari umeporomoka.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW