1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu Tunisia wapinga amri ya rais ya kuingilia mahakama

Sylvia Mwehozi
14 Februari 2022

Maelfu ya raia wa Tunisia siku ya Jumapili waliingia mitaani, kupinga amri yenye utata iliyotangazwa na Rais Kais Saied ya kuingilia uhuru wa mahakama wakisema kuwa ni pigo jingine kwa demokrasia ya nchi. 

Tunesien Proteste
Picha: Hassene Dridi/AP Photo/picture alliance

Amri hiyo iliyochapishwa awali ilimpatia mamlaka makubwa Rais Saied juu ya muhimili wa mahakama na kuanzisha baraza jipya, linalomruhusu kuwatimua majaji na kuzuia uteuzi wao.

Saa chache baadae zaidi ya watu 2,000 waliandamana katika mitaa ya mji mkuu wa Tunis wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo dhidi ya rais. Baadhi walibeba mabango yaliyoandikwa "okoa demokrasia yetu" na mengine yakisomeka "usiguse mahakama". Mmoja ya raia aliyeshiriki maandamano hayo anasema

"Hatutaki mahakama iwe kama ilivyokuwa enzi za Rais wa zamani wa Tunisia Zine El Abidine Ben Ali, watu wote wanasimama na mahakama, watu walio wengi wanakataa udhibiti huu wa mahakama.  Nataka kumwambia rais kwamba watu wanateseka kwa gharama ya juu ya maisha, na hata wale waliopongeza mapinduzi ya Julai 25 wamefuta uungaji mkono wao kwako na bado tunakupa fursa ya kurudi nyuma."

Rais wa Tunisia Kais SaiedPicha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Amri hiyo imetangazwa wiki moja baada ya rais Saied kusema kuwa atalivunja Baraza la juu la mahakama CSM. Hatua hiyo ilisababisha mgomo wa nchi nzima wa majaji wakidai kuwa itaingilia uhuru wao. Rais Saied ameanzisha baraza kuu jipya na la muda lenye wajumbe 21 ambao wanapaswa "kuapa kwa Mungu kulinda uhuru wa mahakama." Tisa kati yao ni wateule wa rais.

Tunisia yatumbukia katika mgogoro wa kikatibaWaliobaki wako chini ya udhibiti wake usio wa moja kwa moja na kwa kuzingatia mamlaka aliyo nayo anaweza kumtimua, "jaji yeyote atakayeshindwa kutimiza wajibu wake kitaaluma". Zaidi amri hiyo inawazuia "majaji wa vyeo vyote kushiriki mgomo au kuchukua hatua za pamoja zinazoweza kuingilia au kuchelewesha utendaji kazi wa kawaida wa mahakama.

Mwishoni mwa mwezi Julai, Tunisia ilitumbukia katika mgogoro wa kikatiba wakati rais huyo alipolivunja bunge, kumfuta kazi waziri wake mkuu na kujiongezea mamlaka Hatua hizo zilikuwa awali zimepongezwa na Watunisia wengi ambao walikuwa wamechoshwa na vyama vya kisiasa vinavyoonekana kugubikwa na ufisadi lakini wakosoaji wake wanasema anaongoza nchi kuelekea tena katika utawala wa kimabavu.

Rais Saied ambaye amefanya mapambano ya rushwa kuwa ajenda yake kuu, amekuwa akisisitiza kwamba hana dhamira ya kuingilia mfumo wa mahakama, lakini makundi ya haki za binadamu na nchi zenye nguvu duniani zimekosoa hatua hiyo. Chama cha majaji wa Tunisia kimesema amri hiyo "inawakilisha ukiukwaji wa wazi wa mgawanyo wa madaraka".

Baraza la CSM ambalo lllianzishwa mwaka 2016 lilikuwa na uamuzi wa mwisho wa uteuzi wa kimahakama. Kwa muada mrefu rais Saied amekuwa aklituhumu baraza hilo kwa kuzuia uchunguzi nyeti wa kisiasa na kushawishiwa na adaui zake.

 

     

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW