1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Cologne kumuunga mkono Erdogan

Mohammed Dahman31 Julai 2016

Polisi wa ziada wamewekwa katika mji wa Cologne, Ujerumani wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika Jumapili (31.07.2016) ya watu wanaomuunga mkono Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki ambayo yamevutia umati wa watu.

Deutschland Köln Pro-Erdogan-Demonstration
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Meissner

Maelfu ya watu wanaomuunga mkono rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki wameandamana mjini Cologne nchini Ujerumani, kufuatia jaribio la mapinduzi liloshindwa Julai 15. Polisi wamesema watu wapatao 20,000 wameshiriki katika maandamano hayo, yaliyoitishwa na makundi yanayomuunga mkono Erdogan ikiwa ni pamoja na Chama cha Wanademokrasia wa Ututuki Ulaya (UFTD).

Maandamano hayo yalianza kwa wimbo wa taifa wa Uturuki na Ujerumani kabla ya waandamanaji kukaa kimya kwa dakika moja kama ishara ya heshima kwa wale waliopoteza maisha katika jaribio la mapinduzi huko Uturuki, mashambulizi ya miji ya Paris pamoja na Munich. Watu 30,000 hadi 50,000 wanatarajiwa kushiriki katika maandamano hayo. Ujerumani ina idadi kubwa ya wakaazi walio na asili ya Kituruki, ambao walikuja kama wafanyakazi katika miaka ya 1960.

Maandamano mengine kadhaa pia yamepangwa kupinga maandamano hayo ya wafuasi wa Erdogan. Serikali inasema polisi 2,700 wakiwemo wale wenye kuzungumza lugha ya Kituruki watamwagwa katika mji huo kuzima makabiliano yoyote yale kati ya makundi yanayopingana.

Mkuu wa polisi wa mji wa Cologne Jürgen Mathies amesema "kitu kimoja ambacho anataka kieleweke bayana ni kwamba wataingilia kati kwa haraka dhidi ya aina yoyote ile ya matumizi ya nguvu kwa uthabiti na kwa nguvu."

Chama cha Wanademokrasia wa Ututuki Ulaya (UFTD) kimeitisha maandamano hayo kulaani jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki lililofanywa na baadhi ya wanajeshi wa Uturuki hapo Julai 15 na kupelekea zaidi ya watu 250 kuuwawa.

Jaribio hilo la mapinduzi limechochea mvutano kati ya wafuasi na wapinzani wa Rais Erdogan ndani ya jamii ya Wuturuki milioni tatu wanaoishi nchini Ujerumani.

Wito wa utulivu

Mbali na maelfu kwa maelfu ya maandamano hayo ya wafuasi wa Erdogan polisi pia inajiandaa kukabiliana pia na maandamano mengine yasiopunguwa manne yenye kupinga maadamano ya wafuasi wa Erdogan ambapo kila kundi la maandamano hayo linatarajiwa kuvutia watu 1,500.Juhudi za polisi kutaka kuzuwiya kundi la sera kali za mrengo wa kulia kushiriki katika maandamano ya Jumapili zimegonga ukuta baada ya mahakama huko Münster kutupilia mbali pingamizi lao hapo Jumamosi.

Jamaa wa waliouawa katika jaribio la mapinduziPicha: Getty Images/K.Bayhan

Kabla ya kufanyika kwa maandamano hayo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steimeier amewahamiza waandamanaji kuonyesha misimamo ya wastani.

Akizungumza na gazeti la Süddeutshe Zeitung amesema sio sahihi kuuleta nchini mvutano wa kisiasa wa Uturuki na kuwatishia watu wenye imani tafauti za kisiasa.

Kiongozi wa chama cha kutetea mazingira cha Green Cem Özdemir pia ameshutumu majiribio hayo yanayodaiwa kuwatisha watu kabla ya kufanyika kwa maandamano hayo ambapo ameiambia kampuni ya habari ya Funke yenye kumiliki magazeti kadhaa nchini kwamba wakosoaji wa Erdogan miongoni mwa jamii ya Waturuki wanaoishi nchini Ujerumani wanaandamwa kwa vitisho.

Amesema "hakupaswi kuanzishwa mazingira ya hofu."

Gokay Sofuoglu mwenyekiti wa jumuiya ya Waturuki nchini Ujerumani amesema familia zimekuwa zikifarakana kutokana na kuwa na utiifu unaokinzana na ametowa wito wa kujiepusha na jazba.

Kuandamwa kwa watuhumiwa

Serikali ya Erdogan imewakamata maelfu ya wanajeshi maafisa katika vyombo vya mahakama, wafanyakazi wa vyombo vya habari na watumishi wa serikali kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa hapo Julai 15 ambapo Sheikh Fethullah Gulen anayeishi uhamishoni nchini Marekani analaumiwa kwa kuwa na mkono wake.

Kikosi maalumu cha jeshi la Uturuki, kikilinda mahakama ya taifa.Picha: Getty Images/C. McGrath

Viongozi wa mataifa ya magharibi wameelezea wasi wasi wao kutokana na hatua za kinidhamu zinazochukuliwa dhidi watu wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi wakati wakosoaji wa Erdogan wana hofu kwamba kiongozi huyo anatumia suala hilo la mapinduzi kama kisingizio ili kuzidi kuimarisha hatamu yake madarakani.

Kabla ya kufanyika kwa maandamano ya Jumapili Erdogan amezitaka serikali za kigeni kutoingilia masuala ya ndani ya Uturuki kwamba "kutojihuisiha na yasiyowahusu".

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/dpa/Reuters

Mhariri : Yusra Buwayhid