Maelfu waandamana duniani kupinga hali mbaya za wafanyakazi
1 Mei 2012Siku hii imevuka mipaka yake ya kuwa siku ya kimataifa ya mapumziko kwa kundi hilo na badala yake imekuwa siku ya kimataifa ya maandamano ya kupinga namna serikali mbalimbali duniani zinavyochukua hatua za kudhibiti mtikisiko wa uchumi kwa mgongo wa wafanyakazi.
Barani Ulaya maelfu ya wafanyakazi wanaandamana mitaani kupinga hatua zinazochukuliwa na serikali katika kudhibiti mtikisiko wa uchumi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia kwenye ongezeko la ukosefu wa ajira.
Huko Marekani, maandamano, migomo na njia za amani za kupinga hali mbaya za wafanyakazi zimepangwa kufanyika ikiwemo kile kinachotazamwa kama maandamano makubwa ya Occupy kuwahi kutokea tangu kuanza kwa maandamano ya Wall Street mwaka uliopita.
Katika Bara la Asia, maelfu ya wafanyakazi kwenye nchi za Ufilipino, Malaysia na Taiwan wanaandamana kudai ongezeko la mishahara ambalo wanasema kuwa halijapanda licha ya kuongezeka kwa gharama za maisha pamoja na kutaka kushushwa kwa gharama za masomo na mambo mengine kadha wa kadha ambayo yanawatatiza.
Mjini Manila Ufilipino kiasi cha wanachama 8,000 wa chama kikubwa cha wafanyakazi nchini humo wanaandamana umbali wa kilometa 4 kuelekea daraja kubwa la Mandiola lililopo karibu na kasri la Rias wa nchi hiyo ambalo limewekewa ulinzi mkali wakiwa wamevalia fulana nyekundu na miamvuli ya kujikinga na jua kali linalowaka kwenye eneo hilo.
Rias wa nchi hiyo Begino Aquino wa tatu amekataa kutimiza masharti ya kilio chao cha kutaka malipo ya dola tatu za Marekani kwa siku akisema kuwa kitendo hicho kitazidisha mfumuko wa bei na kuwafukuza wawekezaji wa kigeni.
Kando na madai hayo, wafanyakazi hao pia wanapinga tabia iliyozoeleka ya makampuni kutoa kazi kwa watu wa nje kwa lengo la kupunguza gharama jambo ambalo linawaumiza wa fanyakazi wa ofisi hizo.
Kuala Lumpur wafanyakazi wanaandamana kutaka nyongeza ya mshahara tofauti na ile iliyotangazwa hivi karibu ni na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Razak.
Ugiriki ambayo imeathirika kwa kaisi kikubwa na mzozo wa kiuchumi, wafanyakazi wake wanaandamana kupinga hatua za kubana matumizi ambazo zinachukuliwa kama sehemu ya kutatua changamoto hiyo inayoikabili. Mvutano huo utauathiri uchaguzi utakaofanyika nchini humo mapema mwezi Juni.
Vyama vikubwa vya wafanyakazi vya nchi hiyo vinatarajiwa kuadhimisha siku hii kwa mitindo tofauti kulingana na mitizamo yao ikiwemo ile ya kikomunisti.
Polisi ya nchi hiyo imejiandaa kudhibiti machafuko yoyote ambayo yamewahi kutokea hapo awali katika maadhimisho ya miaka iliyopita ya siku hii wakati maelfu ya wafanyakazi walipofika mbele ya jengo la bunge nchini humo.
Katika nchi za Uhispania, Ufaransa na Ureno pia vyama vya wafanyakazi vitaendesha maandamano makubwa katika miji mikuu ya nchi hizo kupinga hatua za kubana matumizi na ongezeko la ukosefu wa ajira.
Mwandishi: Stumai George/AFPE/REUTERS/APE
Mhariri: Othuman Miraji