Maelfu waandamana kukumbuka miaka mitatu ya vita vya Yemen
26 Machi 2018Maelfu ya wafuasi wa kundi la waasi wa Houthi wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa leo Jumatatu kukumbuka miaka mitatu ya vita vya nchi hiyoWakati huo huo nchi ya jirani ya Saudi Arabia imesema majeshi yake imeyaangusha makombora saba yaliyorushwa na waasi wa Houthi wa nchini Yemen. Eneo la Sabaeen katika mji wa Sanaa limetanda bendera za Yemeni, na mabango ya picha za kiongozi wa Houthi Abdulmalik al-Huthi au mabango yenye maandishi yaliyosomeka "miaka mitatu ya ukatili".
Mamlaka ya Saudi Arabia imesema mtu mmoja aliyetambuliwa kuwa ni raia wa Misri ameuwawa baada ya kauangukiwa na mabaki ya makombora hayo katika mji wa Riyadh hicho kikiwa ni kifo cha kwanza kutokea tangu muunganowa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulipoingia Yemen mwezi Machi mwaka 2015 ikiwa ni miaka mitatu ya kampeni hiyo yenye lengo la kuirejesha serikali "halali" madarakani baada ya waasi wa Houti na washirika wao kuutwaa mji mkuu wa Sanaa.
Karibu raia wa Yemen 10,000 wameuawa na wengine wapatao 53,000 wamejeruhiwa tangu Umoja wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulipoingia Yemen, na kusababisha kile Umoja wa Mataifa inachokitaja kuwa ni mgogoro mkubwa wa kibinadamu kuwahi kutokea duniani. Waasi wanaoungwa mkono na Iran bado wanaudhibiti upande wa kaskazini mwa mji mkuu wa Yemen, Sanaa pamoja na bandari kubwa zaidi ya nchi hiyo.
Majeshi ya Rais Abedrabbo Mansour Hadi yameudhibiti upande wa kusini mwa Yemen tangu 2015, lakini katika mwaka huu kutokuelewana kumejitokeza kati ya rais Mansour Hadi na washirika wake wa kusini wanaotaka kujitenga.
Majeshi ya Saudi Arabia yalitangaza jana Jumapili usiku kwamba yaliyaharibu makombora hayo saba ya waasi wa Yemeni, yaliyofika katika anga ya mji mkuu wa Riyadh.
Msemaji wa Umoja wa Kijeshi unaoongozwa na Saudi arabia Turki al-Malki amesema "Hatua hii ya kikatili na uadui ya kikundi cha Houthi inathibitisha kwamba utawala wa Irani unaendelea kuwaunga mkono wapiganaji wa kundi hili kwa kuwapa silaha na kuwawezesha kijeshi".
Kituo cha televisheni cha Houthi - Al-Masirah kilidai kuwa waasi hao waliulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa King Khalid wa Riyadh pamoja na viwanja vingine vidogo vidogo vya ndege kusini falme hiyo ya Kiarabu.
Mnamo mwezi Novemba kundi hilo la waasi wa Houthi liliulenga uwanja wa ndege wa Riyadh katika kile ambacho mamlaka ya Saudi ilisema kuwa ni mashambulizi ya kombora ambayo hayakufaulu, hatua iliyosababisha kuanzishwa tena vikwazo vikali dhidi ya bandari za Yemen na uwanja wake wa ndege wa kimataifa. Vikwazo hivyo baadaye viliondolewa kufuatia shinikizo la kimataifa.
Mkuu wa waasi wa Houthi Abdelmalik al-Huthi alisema wapiganaji wake wako tayari kujitoa kafara katika mapambano dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman