1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Maelfu waandamana kupinga mageuzi ya mahakama nchini Israel

11 Julai 2023

Maelfu ya waandamanaji nchini Israel wameteremka mitaani wakiweka vizuizi kwenye njia muhimu kulaani mageuzi ya mfumo wa mahakama ambayo yamesababisha mgawanyiko mkubwa nchini humo.

Israel Tel Aviv | Maandamano dhidi ya mageuzi ya mfumo wa mahakama
Maandamano dhidi ya mageuzi ya mfumo wa mahakama mjii Tel Aviv, Israel Picha: Nir Elias/REUTERS

Israel imeshuhudia wimbi lisilo mfano la maandamano ya umma hii leo yaliyotaziza shughuli za kawaida kwenye miji kadhaa tangu Jerusalem, yaliyo majengo ya bunge hadi mji ulio kitovu cha shughuli za biashara wa Tel Aviv.

Magari yalishindwa kuendelea na safari kwenye njia kadhaa kuu nchini humo baada ya waandamanaji kuweka vizuizi kulaani mageuzi ya mahakama yaliyopendekezwa na utawala wa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu.

Polisi ilitumia magari ya maji ya kuwasha na vikosi vya farasi kujaribu kutawanya makundi ya waandamanaji mjini Jerusalem na Tel Aviv.

Mbele ya majengo ya Bunge huko Jerusalem, waandamanaji walisimama nje wakipeperusha bendera ya taifa huku wakipiga ngoma wakati polisi wakishika doria.

Maandamano yafuatia idhini ya awali kwa mageuzi ya mahakama yenye utata

Waandamanaji walizifunga barabara kuu za miji kadhaa ya Israel Picha: Ilan Rosenberg/REUTERS

Vurumai hiyo imezuka baada ya muungano wa serikali ya waziri mkuu Netanyahu ndani ya bunge kutoa idhini ya awali kwa muswada tata wa sheria wa kuifanyia mageuzi makubwa mahakama ya nchi hiyo, mabadiliko ambayo yamepata upinzani mkali.

Waandamanaji na wafuatiliaji wa siasa za nchi hiyo wanasema mageuzi hayo yatapunguza nguvu za Mahakama Kuu katika kuisimamia serikali.

Mmoja wa waandamanaji aliyejitambulisha kwa majina ya  Ariel Dubinksy alisema; "Tupo kwenye maandamano ya wanasheria dhidi ya kile wanakiita mageuzi, lakini siyo mageuzi ni hatua moja tu kuelekea udikteta. Wanakweda kuharibu, lengo ni kuharibu mfumo wa mahakama kwa kutunga na kutekeleza sheria zitakazosambazatisha demokrasia. "

Muswada uliopata idhini ya awali hii leo ni sehemu ya miswada chungunzima inayopendekezwa na serikali ya Netanyahu na washirika wake wa siasa kali za kizalendo.

Kura iliyopigwa leo inalenga kufuta ibara inayoipa nguvu mahakama kutegua maamuzi ya serikali. Ibara hiyo ilitumika hivi karibuni na mahakama kumlazimisha waziri mkuu Netanyahu kumwondoa kutoka kwenye Baraza lake la Mawaziri mwanasiasa mwanadamizi aitwaye Aryeh Deri kutoka na kutiwa kwake hatiani hapo kabla kwa makosa ya kukwepa kodi.

Upinzani waapa kutopitisha mapendekezo hayo huku serikali ya Netanyahu ikiyatetea

Akizungumza bunge wakati wa mjadala wa usiku kucha kabla ya kupigwa kura leo asubuhi, kiongozi wa upinzani Yair Lapid aliishambulia serikali ya Netanyahu kwa mapendekezo inayoshinikiza yafanyike na kuapa kwamba muswada huo hautapitishwa katika hatua zinazofuata.

Urawala wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu unatetea mageuzi hayo Picha: Maya Alleruzzo/AP/picture alliance

Baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza na kupata idhini leo, muswada huo utapelekwa kwenye ngazi ya kamati ya bunge kama kabla ya kurejeshwa Bungeni kwa uamuzi wa mwisho.

Serikali ya Netanyahu inatetea mapendekezo hayo ikisema ni muhimu kwa sababu mfumo uliopo sasa unatoa madaraka makubwa kwa mahakama. Hayo yalisemwa bungeni na waziri wa sheria Yariv Levin.

Mipango ya mageuzi ilikwama mnamo mwezi Machi baada ya maandamano makubwa ya kuyapinga. Mazungumzo ya kufanya mabadiliko kwenye mapendekezo hayo ili kuondoa vipengele tata yalikwama baada ya upinzani kujitoa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW