1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Sudan kupinga serikali

17 Oktoba 2021

Maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono jeshi, nchini Sudan wamejitokeza mitaani kushinikiza kuvunjwa kwa serikali ya mpito kwa madai kwamba "imefeli " kisiasa na kiuchumi.

Proteste im Sudan
Picha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono jeshi, nchini Sudan wamejitokeza mitaani kushinikiza kuvunjwa kwa serikali ya mpito kwa madai kwamba "imefeli " kisiasa na kiuchumi.

Haya yamejiri wakati kuna mpasuko wa kisiasa Sudan kati ya vikundi vinavyoongoza mchakato wa mpito unaokumbwa na msukosuko, baada ya miongo miwili ya utawala wa mkono wa chuma wa rais wa zamani Omar al-Bashir, aliyeng'olewa madarakani na jeshi Aprili 2019. Soma Waliojaribu mapinduzi Sudan wafungamanishwa na Al-Bashir

Maandamano hayo yameandaliwa na kundi lililogawika la vuguvugu liitwalo Forces for Freedom and Change, FCC, ambalo lilihusika pakubwa kuandaa maandamano dhidi ya Bashir na pia kuwa mshirika mkubwa kwenye mchakato wa mpito. Waandamanaji wameishtumu serikali ya sasa kwa kushindwa kuleta haki na usawa na wanataka serikali itakayoongozwa na jeshi.

"Tunataka serikali itakayoongozwa na jeshi, serikali ya sasa imeshindwa kutuletea haki na usawa," alisema Abboud Ahmed mmoja wa waandamanaji mwenye umri wa miaka 50, karibu na kasri ya rais katikati mwa mji wa Khartoum.

Picha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Serikali ina changamoto

Waziri mkuu Abdallah Hamdok siku ya Ijumaa alionya kwamba serikali ya mpito inakumbwa na changamoto ngumu na hatari.

Kulingana na shirika la habari la SUNA, waandamanaji wamesafiri kwa malori kutoka nje ya mji wa Khartoum kushiriki maandamano hayo.

Wakosoaji wa serikali wamedai kwamba maandamano hayo yamehusisha wafuasi wa utawala wa zamani wa Bashir.

Mabango waliyobeba waandamanaji yalitoa wito wa kuvunjwa kwa serikali. "Jeshi moja, watu wamoja" na "jeshi litatuletea mkate" waandamanaji walinadi kwa sauti. soma Sudan Kusini yaadhimisha miaka 10 ya uhuru

"Tunaandamana kwa amani na tunataka serikali itakayoongozwa na jeshi," alisema Enaam Mohammed, mwanamke mmoja mwandamanaaji.

Mageuzi ya kiuchumi

Picha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Serikali ya mpito imekuwa ikififia katika miezi ya hivi karibuni katika masuala ya mageuzi ya kiuchumi yanayoungwa mkono na shirika la fedha duniani IMF, pamoja na kushuka kwa ruzuku za mafuta na kuzorota kwa thamani ya pauni ya Sudan. soma Ruzuku za petroli na dizeli zasimamishwa Sudan

Maandamano yameghubika mashariki mwa Sudan ambako waandamanaji wamefunga biashara katika bandari ya taifa hilo tangu mwezi Septemba.

Mnamo Septemba 21, serikali ilisema ilizuia jaribio la mapinduzi ambapo liliwalaumu baadhi ya maafisa wa jeshi na raia wanaohusishwa na utawala wa zamani wa Bashir.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW