1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wahamishwa kusini mwa Ujerumani kufuatia mafuriko

3 Juni 2024

Serikali ya Ujerumani imesema kuwa mafuriko mabaya yaliyotokea eneo la kusini mwa taifa hilo yanapaswa kuchukuliwa kama onyo na msukumo wa kuzidisha mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mafuriko katika kijiji cha Fischach karibu na Augsburg huko Bavaria. Kijiji kiko kimefurika maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mafuriko katika kijiji cha Fischach karibu na Augsburg huko Bavaria. Kijiji kiko kimefurika maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Picha: Michael Bihlmayer/Bihlmayerfotografie/IMAGO

Tahadhari hiyo imetolewa wakati maelfu ya watu wakihamishwa na wengine wakilazimika kuyaacha makaazi yao baada ya kutokea mafuriko makubwa mwishoni mwa juma. 

Maafisa wa uokoaji wanaendelea na zoezi la kuwahamisha watu kutoka maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika eneo hilo la kusini mwa Ujerumani huku Kansela Olaf Scholz akieleza kuwa, mafuriko hayo yanapaswa kuchukuliwa kama tahadhari.

Soma pia: Wataalamu waonya kitisho cha mafuriko nchini Ujerumani

Maelfu ya watu katika majimbo ya Bavaria na Baden Wuerttemberg wamelazimika kuyaacha makaazi yao kufuatia mvua kubwa iliyonyesha maeneo hayo tangu siku ya Ijumaa na ambayo imesababisha mafuriko.

Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu wawili – mwokoaji wa kujitolea na mwanamke aliyekutwa amefariki chini ya nyumba ya gorofa.

Scholz aonya juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akitoa shukrani kwa timu ya waokoaji BavariaPicha: Lukas Barth/AFP via Getty Images

Timu ya waokoaji zaidi wameitwa usiku wa kuamkia leo kusaidia katika zoezi la kuhamisha watu kutokana na maji kufurika kupita kiasi. Huko Bavaria, takriban watu 800 wametakiwa kuondoka majumbani mwao katika mtaa wa Ebenhausen-Werk baada ya bwawa kuvunja kingo zake mapema leo.

Kwa upande mwengine wakaazi katika eneo la Manching-Pichl, lililoathirika zaidi na mafuriko wamehimizwa kutafuta hifadhi juu ya gorofa za nyumba zao.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo lililokumbwa na mafuriko kaskazini mwa Munich, Kansela Scholz amesema mafuriko hayo sio "matukio tu ya mara moja.”

Soma pia: Wajerumani walioathirika na mafuriko hawafikirii uchaguzi

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, mafuriko yanayoshuhudiwa Ujerumani ni onyo kwamba inapaswa kuwa macho na kutopuuza kazi ya kuzuia athari ya mabadiliko ya tabia nchi.

"Ukitazama kinachofanyika hapa, watu wangapi waliojitolea kufanyakazi pamoja na maafisa wa uokoaji ambao wamekusanyika kwa muda mfupi tu, utagundua kuwa mshikamano ndio kitu cha muhimu tunachohitaji sisi binadamu na ndicho kinachosaidia wakati wa janga kama hili."

Timu ya uokoaji yatumwa Bavaria

Timu ya uokoaji ikiwahamisha watu kusini mwa Ujerumani.Picha: Daniel Reinelt/Eibner/IMAGO

Gavana wa Bavaria Markus Soeder, aliyeandamana na Scholz katika ziara yake jimboni humo ameeleza kile alichokiita, "hakuna bima kamili” dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Soeder amesema matukio kama hayo yanayofungamanishwa na hali mbaya ya hewa hayakuwahi kutokea miaka ya nyuma. Aidha hali ya hatari imetangazwa katika jimbo lote la Bavaria.

Soma pia: Ujerumani yatakiwa kujiandaa zaidi dhidi ya majanga 

Timu ya uokoaji ya watu 20,000 wamepelekwa Bavaria ili kupambana na athari za mafuriko. Tayari idara ya hali ya hewa ya Ujerumani imetoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea mvua kubwa katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Ujerumani.

Mafuriko hayo na mvua zinazoendelea kunyesha kwa kiasi kikubwa zimeathiri usafiri katika maeneo mengi ya Ujerumani huku safari za treni zikiahirishwa au kufutwa kabisa.

Shirika la reli la Deutsche Bahn limeandika kwenye tovuti yake kuwa njia za treni kutoka Munich hadi Stuttgart, Nuremberg na Wuerzburg zimefungwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW