Maelfu waikimbia Boko Haram
4 Septemba 2014Gazeti la Punch la nchini Nigeria linaripoti kwamba tishio la Boko Haram limewalazimisha zaidi ya watu 26,000 kuyakimbia makaazi yao Kaskazini mwa Nigeria. Pamoja na hayo, gazeti hilo limeishutumu Boko Haram kwa kuwalenga zaidi wanaume kwa nia ya kuwaua. Seneta mmoja wa jimbo la Borno ambalo ni moja ya ngome kuu za Boko Haram amesema kwamba kila mwanaume yuko hatarini kuuliwa na waasi wa kundi hilo.
Wanamgambo wapatao 200 waliripotiwa kuuvamia mji wa Bama uliopo jimboni Borno siku ya Jumatatu. Baada ya mapambano makali na wanajeshi wa Nigeria, wanamgambo 59 waliuliwa huku wengine 30 wakijeruhiwa. Walioshuhudia tukio wanasema kwamba mwishoni Boko Haram ilifanikiwa kuuteka mji wa Bama lakini utawala wa Nigeria umekanusha madai hayo, ukisema kuwa Bama bado iko chini ya serikali ya Nigeria.
Rushwa yatawala
Raia wengi wa Nigeria wametupa lawama kwa serikali yao kwa kushindwa kuwadhibiti waasi wa Boko Haram. Tatizo kubwa linaloelekea kulikabili jeshi la Nigeria ni uhaba wa silaha. Inaaminika kwamba fedha za silaha zipo, lakini hazitumiki jinsi ilivyopangwa kwa sababu ya rushwa. "Wanajeshi hawana silaha. Tukumbuke kwamba miezi michache iliyopita gavana wa jimbo la Borno alikiri kuwa jeshi la Nigeria halina silaha za kutosha. Kama wametoa fedha za kununua silaha kwanini bado maaskari hawana vifaa vya kutosha? Mtu ukinyooshewa bunduki huwezi kupigana kwa vijiti," anaeleza Muhammad Abdul aliyekuwa afisa katika jeshi la Nigeria.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Nigeria, Benin, Cameroon, Chad na Niger wamekutana katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja kutafuta mbinu za kulitokomeza kundi la Boko Haram. Marc-Antoine Pérouse Montclos ni mtaalamu wa masuala ya Nigeria kutoka shirika la ushauri la Chatham House. "Majukumu ya jeshi la Nigeria lazima yabadilike. Jeshi linatakiwa kuwalinda raia. Maaskari wamewafanyia wananchi ukatili mwingi ndio maana wananchi hawataki kushirikiana nao," anaeleza Montclos.
Tangu mwaka 2009, Boko Haram imeua zaidi ya watu 3,000 nchini Nigeria. Kwa mujibu wa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, watu wapatao 700,000 wameyakimbia makaazi yao kwa sababu ya mgogoro kati ya majeshi ya serikali na Boko Haram.
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Iddi Ssessanga