Maelfu waishi bila umeme Ujerumani
11 Desemba 2017Kwa ushirikiano na Shirika la Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi Barani Ulaya (ZEW), shirika la misaada ya kiutu la Caritas limelivalia njuga suala hili na kulifanyia utafiti wa kina. Matokeo ya uchunguzi ambayo yametolewa rasmi hadharani yameonesha hali ilivyo ya kutisha.
Kwa mujibu wa utafiti huo, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kiasi cha familia 328,000 zimelazimika kukatiwa huduma za umeme na wengine milioni 6.6 wakiwa hatarini kufungiwa huduma hiyo muhimu kabisa katika maisha ya kila siku ya binadamu.
Kimsingi kukatiwa umeme ni kitu cha mwisho kabisa kinachofanywa na makampuni ya kutowa huduma hizi ikiwa mtu anashindwa kulipia gharama hizo. Kwanza mtu hupewa muda wa kulipia gharama ya umeme aliotumia endapo alibakisha deni la zaidi ya Euro 100 na mara kadhaa anatumiwa barua ya kumpa onyo na baadaye unatahadharishwa kwamba atakatiwa umeme.
Kwa wengi waliokutwa na hali hiyo, walifungiwa huduma hizi pale tu gharama zilipokuwa zimefikia kiwango kikubwa mno. Si tu wanatakiwa kulipia deni hilo kabla ya kurudishiwa umeme, lakini pia wanatakiwa kulipia tena gharama za kurudishiwa huduma hizo. Ada ya kurudishiwa huduma ya umeme inaweza kufikia hadi Euro 200.
Wanaoathirika ni masikini
Lakini kwa wengi ambao ni watu wanaopokea posho ya serikali ya kuwasaidia kuishi na wale wenye kipato cha chini kabisa nchini Ujerumani, hata kiwango hicho bado ni kikubwa sana kwao na aghalabu hawawezi kukimudu.
Idadi ya watu waliofungiwa huduma ya umeme kwa kipindi cha mwaka mmoja imebakia takriban katika kiwango kile kile. Lakini hadi sasa haijawa wazi ni kina nani hasa ndio waathirika zaidi wa balaa hili.
Suala la kufungiwa huduma za umeme nchini Ujerumani linazitia khofu familia nyingi ambazo ziko hatarini. Na walio wengi kabisa wanaokabiliwa na kitisho hiki ni familia zenye mzazi mmoja, na nyingi zao ni zile zenye kipato kidogo wanaishi chini ya ule mpango unaoitwa "Herz Vier" - posho kwa watu wasiokuwa na ajira.
"Kundi kubwa kabisa lililoingia katika majaaliwa haya ni lile la watu wenye elimu ndogo na ambao wanazongwa na mzigo mkubwa wa madeni na wamekosa kuelewana na idara za serikali zinazohusika," unasema utafiti huo wa Caritas.
Kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba hata familia inayoishi na mtoto mchanga wa miezi sita inakatiwa umeme na malezi ya mtoto huyo kuingia katika hali ngumu na ya hatari.
Lakini kinachotisha na kusikitisha zaidi ni kwamba kwa wengine wanaoishi katika hali hii hulazimika hata mtoto kama huyo kuchukuliwa na familia nyingine itakayomudu kumlea.
Ushauri uliotolewa na ZEW ni kwamba watu wanaoandamwa na madeni wanabidi kutafuta uwezekano wa haraka wa kupata usaidizi. Wanabidi kuanza kutafuta ushauri wa kupambana na madeni. Na juu ya yote watu wanabidi kujifunza kuanza kujisaidia wenyewe kabla ya kuomba msaada..
Mwandishi: Höppner Stephanie/Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef