Maelfu wajitokeza kuiunga mkono serikali Iran
5 Januari 2018Kiongozi aliyeongoza sala za Ijumaa mjini Tehran Ahmad Khatami, ameutaka uongozi wa nchi hiyo kuwaadhibu vikali wale waliohusika katika kuchochea maandamano yaliyopelekea vifo vya zaidi ya watu 22 na zaidi ya watu wengine 1,000 kukamatwa na maafisa wa polisi.
Khatami amesema Wairan wa kawaida waliodanganywa na waandamanaji waliokuwa wanaungwa mkono na Marekani wanastahili kuachiwa huru kulingana na msamaha wa Kiislamu. Muhubiri huyo wa Kiislamu pia ameitaka serikali ya Iran kuangazia matatizo ya kiuchumi yanayowakabili raia wake.
Wakati huo huo Urusi imesema hatua ya Marekani kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya kikao maalum kujadili hali nchini Iran ni jambo linalouingilia uhuru wa nchi hiyo. Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limethibitisha kwamba litafanya kikao hicho Ijumaa.
Rais wa Uturuki ameishutumu Marekani
Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov amesema madai ya Iran kwamba ushawishi kutoka nje ulichochea maandamano lazima yana msingi, na kuongeza kwamba Marekani hutumia mbinu zozote kuzidhoofisha serikali isizozipenda.
Naye Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan ameishutumu Marekani na Israel pia kufuatia hayo maandamano ya siku kadhaa Iran. Vyombo vya habari vya Uturuki hapo awali vilikuwa vimedai kuwa Marekani na Israel zilikuwa zinafuatilia maandamano ya Iran katika harakati za kuifanyia mageuzi kanda ya mashariki ya Kati.
"Haiwezekani sisi kukubali nchi zengine, hususan Marekani na Israel kuingilia masuala ya ndani ya Iran na Pakistan," alisema Erdogan. "Hatua hii ni kuziingilia nchi hizo na inamaanisha kuwachochea watu wa nchi hizo kuzozana baina yao."
Maandamano Iran yalianza Desemba 28
Erdogan hakutoa taarifa zaidi kuhusiana na Marekani na Israel kuiingilia Pakistan katika masuala yake ya ndani ila hapo jana Marekani ilitangaza kusitisha kuipelekea silaha Pakistan pamoja na msaada ya fedha za usalama hadi pale nchi hiyo itakapowachukulia hatua wanamgambo.
Maandamano nchini Iran yalianza Desemba 28 na kuenea kote nchini humo jambo lililopelekea serikali kuifunga mitandao ya kijamii ya Instagram na Telegram iliyokuwa inatumiwa kusambaza picha za maandamano na kuwachochea watu kushiriki.
Wachambuzi wengi wa siasa za Iran wanasema maandamano ya awali yaliyokuwa yanalenga hali ngumu ya kiuchumi ya Iran, yalipangwa na wapinzani wa Rais Hassan Rohani. Lakini mambo yalibadilika baadae na maandamano hayo yakawa yanaulenga uongozi mzima wa Iran ukiwemo utawala wa kidini wa nchi hiyo.
Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel