1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Maelfu wakimbia mapigano Kordofan Kusini

Saleh Mwanamilongo
23 Juni 2023

Nchini Sudan, milipuko iliutikisa kwa mara nyingine mji mkuu wa Khartoum Alhamisi, baada ya kusitishwa kwa mapigano kwa siku tatu. Wakaazi wa Khartoum na miji ya kusini mwa Sudan wanaendelea kukimbia mapigano hayo.

Tschad Flüchtlingscamp Borota Sudan
Picha: Blaise Dariustone/DW

Mashuhuda katika eneo la mashariki mwa Khartoum wameripoti milipuko ya makombora, na mashambulizi makubwa yaliyotokea katika makambi ya jeshi kwenye vitongoji vilivyoko kaskazini mwa mji huo. Kwa upande wao, wakaazi wa mji wa Kadugli ulioko kusini magharibi mwa Sudan walianza kuukimbia mji huo siku ya Alhamisi kufuatia mapigano baina ya jeshi na kundi la SMPLM-N.

Hali hiyo ya taharuki huko Kadugli, mji mkuu wa Kordofan Kusini, na kuongezeka kwa mapigano huko Darfur kunakuja baada ya takriban wiki 10 za mapigano mjini Khartoum, kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF.

''Kiloa mtu alilazimika kukimbia kuokoa maisha yake''

Laura Lo Castro, Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Chad,amesema wanaendelea kupokea wimbi la wakimbizi kutoka Sudan, huku wakiwa katika hali mbovu.

''Walielezea matukio ya kutisha, ambayo kila mtu alilazimika kukimbia kuokoa maisha yake. Kulikuwa na mauaji na kwa hivyo walipokuwa wakikimbia, wakati mwingine kwa bahati mbaya walilazimika kuwaacha watoto wadogo,watu waliojeruhiwa na wazee ambao hawakuweza kukimbia.'', alisema Castro

Jeshi lilishutumu kundi la waasi la SPLM-N linaloongozwa na Abdelaziz al-Hilu, ambaye anadhibiti sehemu za jimbo la Kordofan Kusini, kwa kuvunja makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano na kushambulia kitengo cha jeshi. Jeshi lilisema kuwa lilizima mashambulizi hayo, lakini halikutoa maelezo zaidi kuhusu vifo.

Kusimamishwa kwa mazungumzo ya Jeddah

Picha: Ahmed Satti/Anadolu Agency/picture alliance

Kordofan Kusini ina maeneo makuu ya mafuta ya Sudan na inapakana na Jimbo la Magharibi la Darfur pamoja na Sudan Kusini. Kundi la waasi la SPLM-N lina uhusiano mkubwa na Sudan Kusini, pia lilishambulia jeshi katika mji mwingine wa Kordofan Kusini wa al-Dalanj.

Wakaazi wa Kadugli walisema jeshi limetuma vikosi zaidi kulinda nyadhifa zake mjini huko, huku wapiganaji wa SPLM-N wakiwa wanakusanyika katika maeneo ya pembezoni. Kumeshuhudiwa na hitilafu za umeme na mawasiliano na pia kupungua kwa chakula na vifaa vya matibabu. Vita hivyo pia vimesabisha mlipuko wa ghasia huko Darfur, huku jiji la Darfur Magharibi la El Geneina likiwa limeathirika zaidi.

Mapigano yalishuhudiwa jana kwenye mji wa Al Fashir, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, baina ya jeshi na wapiganaji wa RSF.

Marekani na Saudi Arabia ziliahirisha mazungumzo yanayofanyika mjini Jeddah baina ya pande hasimu nchini Sudan. Marekani imesema muundo wa mazungumzo hayo haufai.

 

Vyanzo Reuters na AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW