1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia mapigano makali Syria

4 Machi 2017

Maelfu ya raia wa Syria wameyakimbia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali  vinayoungwa mkono na Russia na wapiganaji wa jihadi wa kundi lilalojiita Dola la Kiislamu wiki moja iliopita.

Syrien Krieg - Kämpfe in Daraa
Picha: Getty Images/AFP/M. Abazeed

Vikosi vya serikali ya Syria vikisaidiwa na mashambulizi ya anga na mizinga ya Russia vimeendesha mapambano makali dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu na kuviteka takriban vijiji 80 viliokuwa kwenye mikono ya wapiganaji hao wa jihadi tokea katikati ya mwezi wa Januari.

Kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lengo la mashambulizi ya vikosi vya serikali ni kuuteka mji wa Kahafsah unaoshikiliwa na kundi la IS mji ambao una kituo kikuu chenye kusambaza maji kwa mji wa Allepo.

Wakaazi katika mji wa Allepo ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria wamekuwa hawapati huduma ya maji kwa siku 47 baada ya wapiganaji wa jihadi kukata usambazaji wa maji kwa mji huo.Mapigano hayo katika kipindi cha wiki moja yamesababisha wimbi la zaidi ya raia 30,000 kukimbia wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Wengi wakimbilia mji wa Manbij

Miji ya Syria yageuzwa magofu kutokana na mapigano.Picha: picture alliance/abaca/M. Amin Qurabi

Mkuu wa shirika hilo Rami Abdel-Rahman amesema wengi ya watu waliokimbia mapigano hayo wamekwenda kwenye maeneo karibu na mji wa Manbij unaodhibitiwa na vijkosi vya (SDF) washirika wa wapiganaji wa Kikudi na Waarabu wanaoungwa mkono na Marekani ambayo pia inapambana na kundi hilo la IS.

Wengi wao wameshuhudiwa wakielekea katika mji huo kwa kutumia piki piki,mabasi madogo na magari na wengi wao wameonekana kuwa wachovu wakiwa katika misururu kwenye kituo cha ukaguzi kwa jili ya kupekuliwa na kupata ruhusa ya kuingia.

Ibrahim al-Quftan mwenyekiti mwenza wa mamlaka ya kiraia ya mji wa Manbij ameliambia shirika la habari la AFP kwamba takriban watu 40,000 wamewasili katika mji huo katika siku za hivi karibuni.Ameongeza kusema idadi hiyo ya watu waliopotezewa makaazi inaendelea kuongezeka kutokana na mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Syria na kundi la Daesh kama linavyotambulikana kwa Kiarabu (Dola la Kiislam).

Mji waemewa na wimbi jipya la waliopoteza makaazi

Wanajeshi wa Russia wakishiriki mapigano katika mji wa Allepo.Picha: picture-alliance/AP/Russian Defense Ministry

Na kwa mujibu wa Abdel Rahman wa shirika la haki za binaadamu nchini Syria mji huo wa Manbij tayari unawapa hifadhi maelfu ya watu waliopotezewa makaazi ambao waliyakimbia mapigano yaliyopita katika eneo hilo na wanaishi katika mazingira magumu.Amesema hali hiyo itafanya iwe vigumu kwa mamlaka ya mji huo kukaribisha wimbi jipya la watu waliopotezewa makaazi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kushughulikia mahitaji yao ya msingi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza nchini Syria hapo mwezi wa Machi mwaka 2011 zaidi ya nusu ya idadi ya watu wake kabla ya vita hivyo kuanza wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.Mkoa wa kaskazini wa Aleppo una maelfu ya Wasyria waliopotezewa makaazi wengi wao wakiwa katika makambi na mpaka na Uturuki.

Zaidi ya watu 310,000 wameuwawa tokea mzozo huo wa Syria ulipoanza kwa maandamano ya kupinga utawala wa Rais Bashar al-Assad lakini juhudi za kimataifa za kukomesha mzozo hadi sasa zimeshindwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Caro Robi 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW