Maelfu wakimbia mapigano ya M23 Kivu Kusini
8 Mei 2025
Mapigano haya yamesababisha maelfu ya watu kukimbia vijiji vyao na kutafuta hifadhi mjini Bukavu. Katika maegesho ya mabasi na malori, vyombo vyao vya nyumbani kama magodoro, masufuria, na masanduku vimejaa kila kona—ushahidi wa haraka wa kuhama kwao kwa dharura.
Zawadi, mkazi wa kijiji cha Ibambiro katika wilaya ya Walungu, ni mmoja wa waliolazimika kuhama. Anasema walikumbwa na mashambulizi ya ghafla:
"Tuliona watu wanakimbia huku na kule chini ya risasi. Tulijifungia ndani ya nyumba lakini haikusaidia. Nilipoteza watoto wawili, nikaokota mtoto mwingine wa miaka 8. Nawasihi watu wa Bukavu watusaidie,” alisema kwa majonzi.
Hadi sasa, hakuna kambi rasmi iliyoandaliwa kwa wakimbizi hawa wa ndani. Wengi wanahifadhiwa na familia zao mjini Bukavu, huku wengine wakipata hifadhi katika shule na makanisa.
Soma pia:Mzozo wa DR Kongo wavutia idadi inayoongezeka ya washiriki
Lakini hali ya maisha katika mji huo nayo si ya kuridhisha—Benki nyingi zimefungwa, usalama ni wa mashaka, na ajira ni adimu.
Blaise Bisimwa, ambaye alikimbia kutoka kijiji cha Nyangezi, sasa huketi barabarani kila siku akisubiri fursa ya kazi ya mkono: "Maisha ni magumu. Watoto hawasomi tena, kula ni shida. Serikali yetu na M23 wazungumze wapate suluhu ili tuendelee na maisha yetu,” anasema.
Wakimbizi wakumbwa na unyanyapaa, watoto hatarini kiafya
Baadhi ya wakimbizi wanasema wanakumbwa na unyanyapaa kutoka kwa wakazi wa Bukavu. Wengi wao wanashukiwa kuwa washirika wa makundi yenye silaha kutokana na wao kuwa wageni katika vitongoji hivyo.
"Chakula hatupati, hatuna msaada. Hatujafahamika hapa, wanatushuku tu,” alisema mmoja wa wakimbizi waliowasili hivi karibuni. Mwingine akaongeza: "Hapa Bukavu simfahamu mtu. Mungu ndiye anayeniongoza mimi. Ombi langu ni amani ili nirudi nyumbani na watoto wangu.”
Guillaume Munguakonkwa, mjumbe wa kamati ya wakimbizi kutoka kijiji cha Nyangezi, anatoa tahadhari kuhusu hali ya afya ya watoto wachanga: "Watoto chini ya miaka mitano waliokufa ni wengi, takriban 50. Wanakosa huduma za matibabu, na hata wakiwa wagonjwa, hakuna pesa ya kuwapeleka hospitali.”
Soma pia: Marekani imewawekea vikwazo viongozi wa Rwanda na M23
Wakati hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota, mapigano yameripotiwa kuendelea katika vijiji vya Kalonge na Rubemba, eneo la Minembwe wilayani Fizi, kati ya Mai-Mai Wazalendo na wapiganaji wa Twirwaneho wanaoshirikiana na M23/AFC.
Tangu Jumatatu, mapigano zaidi yameshuhudiwa katika maeneo ya Kahamba, karibu na Kamanyola, na waasi wa M23 wameonekana pia katika kijiji cha Luhwindja—eneo maarufu kwa uchimbaji wa madini.