1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia mashambulizi wabeba silaha Nigeria

Angela Mdungu
16 Aprili 2021

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema leo kuwa maelfu ya raia wa Nigeria wanayakimbia mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye silaha na mapigano yanayoendelea kati ya waasi na vikosi vya Nigeria kwenye jimbo la Borno

Nigeria Weltwassertag 2017
Picha: picture-alliance/ZumaPress/UNICEF/Gilbertson

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR  limesema, shambulio la hivi karibuni la waasi lililoripotiwa Jumatano lilisababisha karibu asilimia 80% ya wakazi wa mjini Damasak kukimbia ambao ni karibu watu 65,000 wa eneo hilo.

Msemaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la  kuhudumia wakimbizi  Babar Baloch aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa wabeba silaha hao walishambulia, walipora na kuchoma moto nyumba, maghala ya mashirika ya kutoa misaada, kituo cha polisi, kliniki, na kituo cha shirika la kuhudumia wakimbizi. Baloch amesema, hilo ni shambulio la tatu la ndani ya wiki moja.

Vituo vya kutoa misaada vyalengwa

Naye msemaji wa ofisi ya kuratibu masuala ya kiutu la Umoja wa Mataifa OCHA, Jens Laerke amesema kuna ripoti za kutia hofu za mapigano kati ya wanamgambo na wanajeshi wa serikali ya Nigeria Makundi ya wabeba silaha yamekuwa yakishambulia vituo vya kutolea misaada na wakati mwingine hufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba wakiwatafuta raia wnaofanya kazi kwenye mashirika ya misaada.

Laerke amesema operesheni nyingi za misaada ya kiutu imekuwa ikiahirishwa katika eneo hilo tangu Jumapili kutokana na machafuko."Kama hali hii ikiendelea huenda ikawa ngumu kwetu kupeleka chakula kwa watu wenye uhitaji mkubwa". Ameongeza Laerke.