1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia Niger wakiihofia Boko Haram

5 Mei 2015

Watu wapatao elfu tano wamevikimbia visiwa katika Ziwa Chad kusini-mashariki mwa Niger wakihofia mashambulizi mapya ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo linaandamwa vikali nyumbani nchini Nigeria.

Wakaazi wa visiwa vya Ziwa Chad wakijiandaa kuondoka
Wakaazi wa visiwa vya Ziwa Chad wakijiandaa kuondokaPicha: Reuters/M. Nako

Afisa wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la Ufaransa-AFP, kuwa zaidi ya watu 5,000 tayari wamewasili N'Guigmi, mji ulioko kusini-mashariki mwa Niger unaopakana na Chad. Amesema wengine 11,500 wanatarajiwa kuwasili kwenye mji huo. Wiki iliyopita maafisa wa Niger, waliwataka wakaazi wa maeneo ya karibu na Ziwa Chad kuondoka kwenye visiwa hivyo ifikapo jana Jumatatu, ikihofia uwezekano wa Boko Haram kushambulia visiwa hivyo.

Moussa Tchangari, mkuu wa shirila la Niger lisilo la kiserikali, amesema maelfu ya wanaume, wanawake, watoto na wazee, walitembea umbali wa kilomita 50 hadi kuufikia mji wa N'Guigmi. Tchangari amesema watu hao walikuwa wamechoka kupita kiasi, wana njaa na kiu, wakati walipowasili mjini humo.

Hata hivyo, amesema mji huo haukuwa umeandaliwa kwa ajili ya kuwapokea na kuwasaidia maelfu ya watu hao, shutuma ambazo zimekanushwa na maafisa wa serikali ya Niger. Gavana wa Diffa, amesema leo kuwa kila kitu kinakwenda vizuri. Duru za Umoja wa Mataifa, zimeeleza kuwa serikali imeanza kugawa misaada.

Mmoja wa wanawake waliookolewaPicha: picture alliance/AP Photo

Wakati huo huo Kundi la kigaidi la Boko Haram liko katika hatari ya kuvunjika baada ya mvutano kuzuka kati ya wapiganaji na viongozi wa kundi hilo. Inadaiwa kuwa mvutano huo unachochewa na uhaba wa silaha. Mvutano huo unazuka wakati ambapo majeshi ya serikali yanazidi kusonga mbele.

Wanawake waliookolewa waelezea hali halisi

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa wanawake waliookolewa na serikali kutoka kwa wapiganaji hao wa jihadi, waliokuwa wanashikiliwa mateka tangu mwaka jana. Wamesema wapiganaji wa Boko Haram walikuwa wakiwalalamikia kutokana na uhaba wa bunduki, risasi na mabomu, huku baadhi yao wakitumia fimbo na baadhi ya magari kuharibika au kukosa mafuta na kwamba vikosi vya serikali vinakaribia kulifikia eneo waliko la Sambisa.

Mmoja wa wanawake hao, Salamatu Mohamed amesema siku waliookolewa na wanajeshi wa serikali, wanamgambo hao waligundua kuna helikopta mbili za jeshi zikizunguka kwenye eneo hilo. Anasema baada ya kuona hivyo, wapiganaji hao wakaanza kuwauza kwa Dola 10 kila mmoja. Hata hivyo anasema baadhi ya wanawake walikataa na kuanza kukimbia baada ya kuanza kupigwa kwa mawe.

Msemaji wa shirika la kitaifa la usimamizi wa masuala ya dharura-NEMA katika jimbo la Adamawa, Sa'adou Bello, amesema wanawake 700 pamoja na watoto waliookolewa hivi karibuni wataanza kupatiwa matibabu na wengi wao wanaonyesha dalili za kupatwa na kiwewe.

Wanajeshi wa Nigeria wanaopambana na Boko HaramPicha: Reuters/J. Penney

''Hatutawapeleka moja kwa moja kwenye familia zao, hadi tuwafanyie uchunguzi wa kitaalamu na mtu yeyote atakayekutwa na matatizo atapatiwa matibabu kabla ya kurudishwa,­'' alisema Bello.

Katika miezi ya hivi karibuni jeshi la Nigeria kwa kushirkiana na majeshi ya nchi jirani ya Chad, Cameroon na Niger, yaliripoti kulishinda kundi la Boko Haram baada ya kuwafurumusha kwenye maeneo mengi waliyokuwa wanayadhibiti.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi