1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbilia kusini mwa Gaza kukwepa jeshi la Israel

14 Oktoba 2023

Maelfu ya Wapalestina wamekimbilia eneo la kusini mwa Gaza kusaka hifadhi, baada ya Israel kuwataka waondoke ndani ya masaa 24 kabla ya kuanza operesheni ya ardhini kuwasaka wapiganaji wa Hamas siku ya Jumamosi.

Gazastreifen | Palästinenser auf der Flucht vor dem Krieg
Baadhi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza wakielekea kusini mwa Ukanda huo baada ya kutakiwa na Israel kuondoka kaskazini ndani ya masaa 24 siku ya Jumamosi (Oktoba 14).Picha: Yasser Qudih/Xinhua/picture alliance

Kundi la Hamas, linalotambuliwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kama la kigaidi, limewataka wakaazi wa Gaza kutohama kwenye majumba yao.

Misikiti kwenye ukanda huo imekuwa ikiwatangazia watu wasalie majumbani mwao.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kwamba wiki nzima ya mashambulizi ya mabomu ni mwanzo tu wa operesheni katika Ukanda wa Gaza, baada ya zaidi ya watu 1,300 kuuawa kwenye uvamizi wa Hamas dhidi ya Israel, Jumamosi iliyopita.

Soma zaidi: Viongozi watoa wito wa njia salama kwa wanaohama Gaza

Israel inadai kuwa wengi wa waliouawa, baada ya wapiganaji wa Hamas kuvunja mpaka unaolindwa kwa nguvu kubwa za kijeshi, walikuwa raia wa kawaida. 

Ndani ya masaa 24 yaliyopita, jeshi la Israel linasema lilifanya msako ndani ya Gaza kujaribu kuwaondosha wale linaowaita "magaidi" na kugunduwa walipo watu waliopotea, likimaanisha mateka waliochukuliwa na Hamas.

Baadhi ya Wapalestina wakiondoka upande wa kaskazini mwa Gaza kuelekea kusini ya ukanda huo baada ya Israel kuwapa masaa 24 kuhama.Picha: Hatem Moussa/AP/picture alliance

Hadi sasa, watu zaidi ya 1,900, wengi wao raia na zaidi ya 600 kati yao wakiwa watoto, wameshauawa kwenye wimbi la makombora ya Israel yanayotupwa Gaza, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Palestina.

Jeshi la Israel linasema Hamas iliwachukuwa mateka watu wapatao 150, wakiwamo raia wa Israel, wageni na wale wenye uraia wa nchi mbili na kuenda nao upande wa Gaza.

Kundi hilo la wanamgambo lilisema siku ya Ijumaa (Oktoba 13) kwamba 13 kati ya mateka hao wameuawa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Bearbock, ambaye aliitembelea Israel jana Ijumaa, alisema Hamas inawatumia wakaazi wa Gaza kama "ngao".

Hali yazidi kuwa mbaya Gaza

Israel imeukatia Ukanda huo huduma zote muhimu, yakiwemo maji, mafuta, umeme na chakula. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameilezea hali kwenye Ukanda huo kwamba imefika kiwango cha hatari kubwa, na ametowa wito wa Umoja huo kupatiwa fursa ya kuingia kusambaza misaada ya kibinaadamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametowa wito kwa umoja wake kupatiwa fursa ya kuingia Ukanda wa Gaza.Picha: Craig Ruttle/AP/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye nchi yake ni muungaji mkono wa Israel, amesema hali ya kibinaadamu inapewa kipaumbele.

Hali ya wasiwasi imezuka kote Mashariki ya Kati na maeneo mengine, huku waandamanaji wenye hasira wakijitokeza mitaani kuwaunga mkono Wapalestina, nchini Lebanon, Iraq, Iran, Jordan na Bahrain.

Katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi, Wapalestina 16 waliuawa na wanajeshi wa Israel wakati wakiandamana kuwaunga mkono wenzao wa Gaza, ilisema wizara ya afya.

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestina, Mohammad Shtayyeh, ameituhumu Israel kwa kuendeleza "mauaji ya kimbari" kwenye Ukanda wa Gaza, lakini msemaji wa Netanyahu, Tal Heinrich, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "kinachotokezea Gaza ni makosa ya Hamas."

Vyanzo: Reuters, AFP