1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu walikimbia eneo la kaskazini mwa Burkina Faso

Sylvia Mwehozi
9 Juni 2021

Burkina Faso imesema kwamba zaidi ya watu 7,000 wamelikimbia eneo la kaskazini lililokumbwa na machafuko kufuatia mauaji makubwa ya hivi karibuni katika uasi uliodumu kwa miaka sita sasa

Burkina Faso Symbolbild Anschlag
Picha: Str/AFP

Waziri mkuu wa taifa hilo Christophe Dabire amesema tayari hatua zimechukuliwa kuwasaidia watu waliokosa makaazi kwa kuwapatia kiwango cha chini cha faraja, malazi na chakula huku akiahidi ziara katika eneo lilipofanyika shambulizi na kuapa kuwawajibisha wahusika.

Washauri wake wamelieleza shirika la habari la AFP kuwa watu 7,600 wamekimbilia Sebba, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Yagga ulioko kilometa 15 kutoka kijiji cha Solhan kulipofanyika mashambulizi.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, Babar Baloch alisema kuwa zaidi ya watu 3,300 walikimbia wakiwemo watoto 2,000 na zaidi ya wanawake 500 baada ya washambuliaji kuvamia kijiji hicho siku ya Jumamosi na kuwaua raia wapatao 160. Shambulio hilo linatajwa kuwa baya tangu uasi ulipozuka katika taifa hilo la Afrika Magharibi mwaka 2015.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alisema kuwa hivi sasa vikosi vya kupambana na makundi ya jihadi vinaendesha operesheni katika maeneo ya mipaka baina ya Burkina Faso, Mali na Niger.

Jeshi la Ufaransa likipiga doria Burkina Faso 2019Picha: Michel Cattani/AFP

"Burkina Faso ni sehemu ya kikosi cha pamoja cha nchi za ukanda wa Sahel zinazojulikana kama G5 na tunaendelea na operesheni za kijeshi wakati huu katika eneo la mpaka wa nchi tatu kwa uratibu wa karibu na majeshi ya washirika na kikosi cha pamoja cha G5. Lakini tukio hili limetuonyesha kwamba hatua za kijeshi hazitoshi ikiwa majimbo hayatodhibiti maeneo yake"

Washambuliaji walichoma karibu kila kitu katika kijiji hicho ikiwemo nyumba, masoko, shule na vituo vya afya. Mauajihayo yanafuatia mengine ya watu 14 yaliyofanyika siku ya Ijumaa kwenye kijiji cha Tadaryat katika mkoa huo huo, ambao wanajihadi wenye mafungamano na makundi ya Al-Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS wamekuwa wakiwalenga raia na askari.

Kwa mujibu wa UNHCR, watu waliokimbia wanahitaji msaada wa haraka wa maji, malazi na huduma za matibabu.Tangu mwaka 2015 Burkina Faso imeshuhudia ongezeko la ghasia kutoka kwa makundi ya wanajihadi, ikiwemo kundi linalounga mkono Uislamu na Waislamu la GSIM pamoja na kundi jingine la EIGS katika ukanda wa Sahara.

Hata hivyo, kundi la GSIM hapo jana lilikanusha kuhusika na shambulizi la Solhan na kulaani mauaji hayo kama ya "kutisha". Baraza la usalama la umoja wa mataifa "lililaani kwa nguvu zote" shambulio hilo na kuongeza kuwa "ugaidi katika aina zote ni mojawapo ya vitisho vikali kwa amani na usalama wa kimataifa".

Mashambulizi ya wanajihadi nchini Burkina Faso yalianza eneo la kaskazini karibu na mpaka na Mali mwaka 2015 lakini tangu wakati huo yameenea katika mikoa mingine hususan mashariki. Watu wapatao 1,400 wameuwawa na karibu milioni 1.2 kukosa makaazi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW