1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya waomba hifadhi waandika maombi zaidi ya mara mbili

Saumu Mwasimba
1 Desemba 2019

Data zaonesha maelfu ya wakimbizi waliorudishwa,au kuondoka kwa hiyari Ujerumani warudi tena kuomba hifadhi zaidi ya mara mbili

Symbolbild BAMF
Picha: Getty Images/S. Gallup

Data za serikali ya Ujerumani zinaonesha kwamba maelfu ya waomba hifadhi wanaoishi nchini Ujerumani walirudishwa,au kuondoka kwa hiyari nchini kabla ya kurudi tena na kuomba upya hifadhi. Hayo yamebainika kupitia ripoti iliyochapishwa na gezeti la Welt am Sonntag la hapa Ujerumani.

Kufikia October 30 mwaka 2019 walikuwepo waomba hifadhi 4,916 nchini Ujerumani ambao waliwahi kuingia nchini humu mara mbili tangu mwaka 2012 na baadaye walirudishwa makwao au kuondoka kwa hiyari na kisha kurudi tena kwa mara nyingine na kuandika maombi kwa mara ya tatu.

Picha: Imago/IPON

Kuna watu 1,023 wanaoomba hifadhi wanaoishi nchini Ujerumani ambao wanajaribu kwa mara ya nne kuomba hifadhi. Jumla ya waomba hifadhi 294 wamejaribu kufanya hivyo mara tano au zaidi. Idadi hiyo ni jumla ya idadi ndogo ya wale waliotuma maombi yao ya kuomba hifadhi nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa Ofisi ya serikali kuu kuhusu Data watu milioni 1.78 waliingia Ujerumani wakiomba hifadhi ya ukimbizi kati ya mwaka 2010 na 2018.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer ametowa mwito wa kuwepo mageuzi barani Ulaya kuhusu wanaoomba hifadhi ikiwemo kuanzishwa utaratibu maalum wa kufanyika uchunguzi wa awali wa maombi ya wahamiaji wanaoomba ulinzi kabla ya kuingia barani Ulaya.

Alitangaza hatua za Ujerumani kudhibiti mipaka wiki kadhaa zilizopita kama hatua ya kukabiliana na visa vya wahamiaji waliokataliwa nchini Ujerumani kurudi tena kama kisa kilichotokea hivi karibuni kinachomuhusu kiongozi wa kundi la kilebanon la Miri aliyeingia Ujerumani. Ibrahim Miri alirudishwa kwao Lebabon mwezi Julai baada ya kuhukumiwa kwa makosa ya uhalifu unaohusisha mihadarati lakini akaingia tena Ujerumani katika mji wa bandari wa Kaskazini wa Bremen mwishoni mwa mwezi October.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Tatu Karema