Maelfu warejea Gaza baada ya usitishaji mapigano
11 Oktoba 2025
Maumi kwa maelfu ya Wapalestina waliochoka wameanza kurejea katika nyumba zao zilizoharibiwa siku ya Jumamosi, siku moja baada ya usitishaji mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas kuanza kutekelezwa Gaza.
Shirika la habari la Reuters lilielezea msururu mkubwa wa watu wakisafiri kwa miguu kuelekea kaskazini, wakipitia barabara ya pwani kando ya fukwe kuelekea Jiji la Gaza, eneo kubwa zaidi la nchi kavu katika ukanda huo.
Hadi Ijumaa alasiri, jiji hilo lilikuwa shabaha ya moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya Israel katika vita hiyo.
Msemaji wa shirika la ulinzi wa raia wa Gaza, Mahmud Bassal, alisema takriban Wapalestina 200,000 wamekwisha rejea kaskazini mwa Gaza tangu usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa.
Wakazi wa Gaza warejea kwenye magofu
"Namshukuru Mungu nyumba yangu bado imesimama," alisema Ismail Zayda katika mtaa wa Sheikh Radwan, Jiji la Gaza. "Lakini eneo lote limeharibiwa, nyumba za majirani zangu zimebomolewa, mitaa mizima imetoweka."
Mpalestina mwingine, Mahdi Saqla, alisema familia yake iliamua kuelekea kaskazini kwenda Jiji la Gaza mara tu waliposikia habari za usitishaji mapigano.
"Hakuna nyumba — zote zimeharibiwa," alisema. "Lakini tunafurahi kurudi mahali ambapo nyumba zetu zilikuwepo, hata kama ni juu ya magofu. Hiyo pia ni furaha kubwa. Kwa miaka miwili tumeteseka, tukihama kutoka sehemu moja hadi nyingine."
Katika eneo la kusini la Khan Younis, ambalo hapo awali lilikuwa jiji la pili kwa ukubwa katika ukanda huo, mamia ya Wapalestina waliorejea walikuta majengo yakiwa yamebomolewa, magofu na uharibifu mkubwa baada ya wanajeshi wa Israel kuondoka katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.
"Hakuna kilichosalia. Ni nguo chache tu, vipande vya mbao na sufuria," alisema Fatma Radwan, mkazi aliyehamishwa, katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, akiongeza kuwa watu bado wanajaribu kuondoa miili kutoka chini ya magofu.
Mkazi mwingine wa Khan Younis, Ahmed al-Brim, alisema aliweza kupata mbao tu kutoka kwenye magofu ya nyumba yake, ambazo atazitumia kama kuni za kupikia.
"Tulirudi katika eneo letu. Limefutwa kabisa. Hatujui tutakwenda wapi baada ya hapo," alisema. "Hatujaweza kupata samani, nguo, au kitu chochote — hata nguo za baridi. Hakuna kilichobaki."
Israel yaondoa wanajeshi wake
Wapalestina walisema mashambulizi makali katika maeneo ya Gaza mapema siku ya Ijumaa yalikuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa baada ya tangazo la usitishaji mapigano kutoka kwa jeshi la Israel.
Shirika la ulinzi wa raia wa Gaza lilithibitisha kuwa wanajeshi wa Israel na magari ya kivita walikuwa wakijiondoa kutoka uwanja wa mapigano katika Jiji la Gaza na Khan Younis.
Hata hivyo, Israel ilitoa onyo kwa Wapalestina kujiepusha na vikosi vyake wakati wakifanya "marekebisho ya nafasi za operesheni."
Wizara ya Mambo ya Ndani inayoendeshwa na Hamas ilisema inatuma vikosi vya usalama katika maeneo ambayo jeshi la Israel limeondoka.
Usambazaji wa misaada kuongezwa
Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa umepewa idhini na Israel kuanza kusambaza misaada kwa kiwango kikubwa zaidi kuanzia Jumapili, afisa wa Umoja wa Mataifa alisema kwa sharti la kutotajwa jina.
Msaada huo utajumuisha tani 170,000 za vifaa ambavyo tayari vimehifadhiwa katika nchi jirani kama Jordan na Misri.
Msaada huo unalenga kukabiliana na utapiamlo mkali na hali ya njaa, ambayo imezidi kuwa mbaya kutokana na vikwazo vya Israel kuhusu upatikanaji wa misaada wakati wa vita.
Katika miezi michache iliyopita, UN na washirika wake wameweza kusambaza asilimia 20 tu ya misaada inayohitajika Gaza, kwa mujibu wa mkuu wa misaada ya kibinadamu wa UN, Tom Fletcher.
Watu wa Gaza bado wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa kiwango cha juu, alisema Tess Ingram, meneja wa mawasiliano wa shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, katika mahojiano na DW.
"Kama watu wanarudi kwenye uharibifu tunaoufahamu, watahitaji msaada mkubwa. Watahitaji maji safi ya kunywa, watahitaji makazi," alisema Ingram.
"Majira ya baridi yanakaribia, hivyo hali ni ya hatari sana," aliongeza. "Baridi imeanza na mvua zinatarajiwa katika siku au wiki chache zijazo. Kwa hiyo tunajaribu pia kuleta blanketi kwa watoto, nguo za baridi na viatu. Ni jambo la kusikitisha kuona watoto wengi wakitembea juu ya magofu bila viatu."
Maswali mengi yanasalia bila majibu kuhusu mpango wa amani
Licha ya sherehe zilizofanyika Israel na Gaza kufuatia kuanza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza ya mpango wa amani wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani Donald Trump, masuala mengi bado hayajatatuliwa, yakiwemo suala la Hamas kuachana na silaha na mamlaka ya mpito iliyopendekezwa kwa Gaza ambayo ingeongozwa na Trump, huku Tony Blair, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, akipewa nafasi kubwa.
Mpango huo unataka Israel iendelee kuwepo kijeshi ndani ya maeneo ya Wapalestina bila kikomo, hasa katika mpaka wake na Israel.
Jeshi la kimataifa, litakalojumuisha kwa kiasi kikubwa wanajeshi kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu, litakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama ndani ya Gaza.
Hata hivyo, Hamas ilitoa tamko Ijumaa jioni ikikataa kile ilichokiita "ulinzi wa kigeni," na kuongeza kuwa uongozi wa Gaza ni suala la ndani la Wapalestina pekee.
Chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano, Hamas itakabidhi mateka 48 waliobaki, ambapo 20 kati yao wanadhaniwa kuwa bado hai. Wanatarajiwa kuachiliwa ndani ya siku chache zijazo.
Vita ya Gaza vya miaka miwili vilichochewa na mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 1,200 na kutekwa kwa watu 251.
Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya Wapalestina na kuwahamisha takriban asilimia 90 ya wakazi wa Gaza wapatao milioni 2, mara nyingi zaidi ya mara moja.
Vyanzo: AP, AFP, Reuters