1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Maelfu wauaga mwili wa Papa Mstaafu, Benedict XVI

2 Januari 2023

Maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki wamejitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Papa Mstaafu Benedict XVI katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter. Papa alifariki dunia siku ya Jumamosi akiwa na umri wa miaka 95.

Vatikan Aufbahrung Papst Benedikt
Picha: Vatican Media via REUTERS

Waombolezaji watapata muda wa siku tatu kuuaga mwili wa kiongozi huyo wa zamani wa Kanisa Katoliki duniani. Waumini hao walipanga foleni kuanzia alfajiri ya Jumatatu kuuaga mwili wa mwanateolojia huyo wa Kijerumani, ambao asubuhi Jumatatu uliondolewa katika Monasteri ya Mama wa Kanisa na kupelekwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter mjini Vatican. Benedict ameliongoza Kanisa Katoliki kwa takribani miaka minane, kabla ya kuwa papa wa kwanza katika karne sita kujiuzulu mwaka 2013, kutokana na hali yake ya afya kudorora.

Mrithi wake, Papa Francis ataongoza Ibada ya mazishi yake itakayofanyika kwenye Viwanja vya Mtakatifu Peter siku ya Alhamisi, kabla ya mwili wake kuzikwa katika makaburi yaliyoko chini ya kanisa hilo.

Tukio la heri na kinyenyekevu

Padri George Ngosa kutoka Zambia aliyekuwa miongoni mwa waumini waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho, anasema amefanikiwa kuuona mwili huo ukiwa umevikwa mavazi ya Kiaskofu na hivyo hilo ni tukio la kheri.

''Nadhani unajua ni tukio la mara moja katika maisha, kujionea mwenyewe Papa akiwa amelala ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter. Ni jambo la kheri, lakini pia ni jambo la mimi kujinyenyekeza kama kasisi kupata nafasi hii hapa Roma,'' alisema Padre Ngosa.

Vatican imetenga muda wa saa 10 kwa siku ya Jumatatu watu kutoa heshima zao za mwisho. Siku za Jumanne na Jumatano muda uliotengwa ni wa saa 12, kabla ya ibada ya mazishi itakayofanyika Alhamisi asubuhi.

Watu wakiwa wamejipanga mstari wakisubiri kuingia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter kuuaga mwili wa Papa Mstaafu Benedict XVIPicha: Ciro De Luca/REUTERS

Rais wa Italia, Sergio Mattarella na Waziri Mkuu Giorgia Meloni, ni miongoni mwa watu waliojitokeza Jumatatu kutoa heshima zao za mwisho kwa Papa Mstaafu Benedict XVI, baada ya milango kufunguliwa majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za Vatican. Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter, Agnello Stoia, ameliambia shirika la habari la ANSA kwamba katibu wa muda mrefu wa Benedict, Askofu Mkuu Georg Gaenswein, alikutana na viongozi wote hao wawili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter.

Watu 60,000 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Benedict

Maafisa wa usalama wa Italia wamesema wanatarajia zaidi ya watu 25,000 watatoa heshima zao za mwisho katika siku ya kwanza, na huenda watu 60,000 watahudhuria mazishi ya Benedict. Wakati papa wa zamani John Paul II alipofariki mwaka 2005, mamilioni ya waumini walihudhuria mazishi yake, wakiwemo marais, mawaziri wakuu na wafalme kutoka zaidi ya nchi 100 duniani.

Kwa upande wa mazishi ya Benedict, Vatican imezialika nchi za Italia na Ujerumani pekee kutuma wajumbe rasmi, na kuzishauri balozi za kigeni kwamba viongozi wengine wowote wanaotaka kuhudhuria mazishi hayo, wanaweza kufanya hivyo lakini kwa ''uwezo wao binafsi.''

Kwa mujibu wa taarifa za awali za Vatican hakutokuwa na shughuli kubwa sana ya mazishi ya Benedict, kwa lengo la kuenzi matakwa yake, ya kuwa na mazishi ya kawaida, lakini pia kuweka wazi kwamba kutokana na yeye kuwa papa mstaafu hafai kufanyiwa mazishi yenye hadhi sawa na papa anayefia madarakani.

(AFP, AP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW