1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wazikimbia nyumba zao kuepuka moto wa msituni Ugiriki

Daniel Gakuba
6 Agosti 2021

Maelfu ya watu wamekimbizwa kutoka makaazi yao yaliyokuwa yakitishiwa na moto karibu na mji mkuu wa Ugiriki, Athens, wakati wafanyakazi wa kuzima moto wakifanya kila juhudi kunusuru majengo na miondombinu ya umeme.

The Day in Pictures | Griechenland Waldbrände bei Drossopigi
Picha: Eurokinissi/ZUMA Wire/imago images

Walinzi wa pwani ya Ugiriki wamefanya operesheni kubwa kunusuru mamia ya wakaazi na watalii waliokuwa wamepiga kambi katika kisiwa cha Evia, huku moto mkubwa ukiendelea kuteketeza maeneo mengi kote Ugiriki kwa siku ya tatu mfululizo leo.

Hata hivyo sio wote wanakubali kuondoka, kama anavyosema Giannis Kanellopoulos, mzee wa miaka 71 aliyekaidi kukimbilia mahali salama akiiacha nyuma nyumba yake.

''Wanasema tuondoke? Tuondoke twende wapi? Siwezi kuondoka niiache nyumba yangu iungue moto. Kama tungeondoka sehemu hii yote ingekuwa imeteketea,'' amelalama mzee Kanellopoulos na kuongeza kuwa wamewaambia wanawake na wazee na watoto waende, lakini yeyote mwenye nguvu alibaki hapa akisaidia kwa namna yoyote anavyoweza.

Mojawapo ya ndege zilizopelekwa kusaidia katika shughuli ya kuuzima moto huu wa msituni UgirikiPicha: INTIME/REUTERS

Mamia ya nyuma za makaazi ya watu zateketezwa

Moto mkubwa zaidi umepita katika msitu ulioko umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa mji wa Athens na kuharibu kabisa nyumba nyingi za makaazi ya watu.

Soma zaidi: Moto wa msituni watishia miundombinu Ugiriki na Uturuki

Shughuli za usafiri katika barabara kuu inayouunganisha mji wa Athens na mikoa ya kaskazini zimetatizika kutokana na kazi ngumu ya kuuzima moto huo iliyowahusisha mamia ya wazima moto waliosaidiwa na magari maalumu na ndege zinazomwaga maji na kemikali kutokea angani.

Maafisa kadhaa wa zimamoto pamoja na wale wa kujitolea wamepata majeraha ya moto na kukimbizwa hospitali. Waziri wa afya wa Ugiriki Vassilis Kikilias amethibitisha kuwa watu tisa walibebwa na gari la wagonjwa k´hadi hospitali moja ya kaskazini mwa mji wa Athens, baadhi yao wakiwa na matatizo ya upumuaji.

Kondoo hawa wamekusanywa mahali penye usalama katika kisiwa cha EuboeaPicha: Thodoris Nikolaou/AP/dpa/picture alliance

Kamanda wa vikosi vya wazimamoto, Brigedia Jenerali Aristotelis Papadopoulos amesema Ugiriki inapita katika kipindi cha siku kumi za mawimbi ya joto, makali zaidi kwa viwango na muda yatakaodumu ikilinganisha na mengine yote ya miaka 30 iliyopita.

Msaada wawasili kutoka Umoja wa Ulaya

Leo hii vikosi vya msaada na vifaa vinatarajiwa kuwasili nchini Ugiriki kutoka Uswisi, Sweden, Romania na Ufaransa, na vile kutoka Cyprus tayari vimefika.

Soma zaidi: Moto waua watu 50 Ugiriki

Nako nchini Uturuki ambako kwa muda wa majuma matatu yaliyopita moto umeuwa watu wanane na kuharibu mali nyingi, serikali ya rais Recep Tayyip Erdogan imekabiliwa na ukosoaji, kwamba haikufanya vya kutosha kupambana na moto huo kwa kutumia raslimali iliyotengwa kwa ajili hiyo.

Takwimu zilizopatikana hivi karibuni zimeonyesha kuwa idara ya misiti ya nchi hiyo ilitumia asilimia mbili tu ya bajeti yake ya dola milioni 24 ilizopatiwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuzuia moto na kununua vifaa vya kupambana na moto pale unapozuka misituni.

 

rtre, ape

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW