1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya raia wa Sudan wakimbia machafuko ya El Fasher

3 Novemba 2025

Maelfu ya watu wameikimbia miji na vijiji katika machafuko yanayoendelea mashariki mwa Darfur. Umoja wa Mataifa umetoa taarifa hiyo ikiwa ni zaidi ya wiki moja tangu wanamgambo wa RSF walipoudhibiti mji wa El Fasher.

Sudan Tawila 2025 | Raia wa Sudan wakimbia machafuko ya El Fasher
Maelfu ya raia wa Sudan wakimbia machafuko ya El Fasher Picha: AFP

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, limesema linakadiria kuwa zaidi ya watu 36,825 wameikimbia miji huko Kordofan Kaskazini, eneo ambalo ni zaidi ya kilomita 100 kutoka Mashariki mwa mkoa wa Darfur.

Katika eneo hilo ndiko vikosi vya RSF vilipoidhibiti ngome ya mwisho kubwa zaidi ya jeshi.

Kwengineko Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV amerejelea wito wake wa kutaka mapigano kusitishwa haraka Sudan ili misaada ya kibinaadamu ipelekwe katika eneo hilo lililokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vita hivyo vya kung'ang'ania madaraka Sudan, vilianza Aprili mwaka 2023, kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali  Abdel-Fattah al Burhan na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.