1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya raia wa Ukreni wazuwiliwa katika magereza ya Urusi

14 Julai 2023

Maelfu ya raia wa Ukreni wanazuiliwa kote nchini Urusi na maeneo ya Ukreni yanayokaliwa, katika vituo vya kuanzia maeneo mapya ya magereza ya Urusi hadi vyumba vya chini vya ardhi.

Ukraine I  a new investigation from Kherson
Picha: Igor Burdyga/DW

Waraka wa serikali ya Urusi wa kuanzia mwezi Januari unaainisha mipango ya kuunda makoloni mapya 25 ya magereza na vituo vingine sita vya kuzuwilia katika maeneo yanayokaliwa nchini Ukreni kufikia 2023.

Raia wengi wanashikiliwa kwa makosa madogo kama vile kuzungumza Kiukreni au kuwa kijana katika eneo linalokaliwa, na mara nyingi wanashikiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Wengine wanashtakiwa kama magaidi, wapiganaji, au watu wanaopinga operesheni maalum ya kijeshi.

Soma pia: Mashambulizi nchini Urusi yaharibu dhana ya 'jeshi la Putin'

Mamia hutumiwa kwa kazi za utumwa na jeshi la Urusi, kuchimba mitaro na ngome nyengine, pamoja na makaburi ya halaiki. Mateso ni jambo la kawaida, yakijumuisha kurushwa kwa umeme, vipigo vinavyosababisha kuvunjika mafuvu na mbavu, na simulizi la kukosa hewa.

Moja ya jela walimokuwa wakizuwiliwa raia wa Ukreni katika mkoa wa Kherson wakati mkoa huo ulipokuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Urusi.Picha: Igor Burdyga/DW

Wafungwa wengi wa zamani waliiambia AP kuwa walishuhudia vifo. Ripoti ya Umoja wa Mataifa kutoka mwishoni mwa Juni iliorodhesha matukio 77 ya  mauaji ya kinyume cha sheria ya mateka wa kiraia na kifo cha mtu mmoja kutokana na mateso.

Urusi haikiri kuwashikilia raia hata kidogo, achilia mbali sababu zake za kufanya hivyo. Lakini wafungwa hao wanatumika kama kikomboleo katika mabadilishano na askari wa Urusi, na Umoja wa Mataifa umesema kuna ushahidi wa raia kutumika kama ngao za binadamu karibu na mstari wa mbele katika mapigano.

Soma pia: Maoni: Uvamizi wa Urusi Ukraine unamhusu kila raia wa Ulaya

AP ilizungumza na makumi ya watu, wakiwemo wafungwa 20 wa zamani, pamoja na wafungwa wa zamani wa vita, familia za zaidi ya raia kumi na mbili walioko kizuizini, maafisa wawili wa ujasusi wa Ukraine na mpatanishi wa serikali.

Ukiukaji wa mikataba ya Geneva

Maelezo yao, pamoja na picha za satelaiti, mitandao ya kijamii, nyaraka za serikali na nakala za barua zilizowasilishwa na Shirika la Msalaba Mwekundu, vinathibitisha mfumo mpana wa Urusi wa kuwaweka kizuizini na kuwanyanyasa raia ambao unakiuka moja kwa moja Mikataba ya Geneva.

Baadhi ya vyumba vya mateso wanamozuwiliwa wafungwa wa kiraia wa Ukreni katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi.Picha: Igor Burdyga/DW

Baadhi ya raia walizuiliwa kwa siku au majuma kadhaa, huku wengine wakitoweka kwa zaidi ya mwaka mmoja. Takriban kila mtu aliyeachiliwa walisema alipitia au alishuhudia mateso, na wengi walieleza kuhamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine bila maelezo. Ni biashara ya ulanguzi wa binadamu," alisema Olena Yahupova, msimamizi wa mji alielazimishwa kuchimba mitaro kwa ajili ya Warusi mkoani Zaporizhzhia.

Soma pia: Hungary: Je Orban ana tatizo gani na Ukraine?

Takriban raia 4,000 wanashikiliwa nchini Urusi na wengi pia wametawanyishwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, kulingana na Vladimir Osechkin, mwanaharakati wa haki za binadamu wa Urusi aliyeko uhamishoni, ambaye anazungumza na watoa habari ndani ya magereza ya Urusi na mwanzilishi wa mtandao wa Gulagu.net unaoorodhesha matukio ya ukiukaji.

Viongozi wa Afrika wataka kumaliza mzozo wa Ukraine

02:31

This browser does not support the video element.

Osechkin aliionyesha AP waraka wa gereza wa Urusi kutoka 2022 ukisema kwamba watu 119 ''waliopinga operesheni maalum ya kijeshi'' nchini Ukraine walihamishwa kwa ndege hadi koloni kuu la magereza katika eneo la Urusi la Voronezh. Waukraine wengi walioachiliwa baadaye na Urusi pia walielezea uhamishaji wa ndege ambao haujaelezewa.

Kwa ujumla, serikali ya Ukraine inaamini takriban raia 10,000 wanaweza kuwa wanazuiliwa, kulingana na mpatanishi wa Ukraine Oleksandr Kononeko, akinukuu ripoti za wapendwa, pamoja na mahojiano na walioachiliwa, na baadhi ya raia na mamia ya askari wa Ukraine waliorudi kupitia mpango wa kubadilishana wafungwa.

Chanzo: AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW