Maelfu ya wafungwa waachiwa huru Morocco
30 Julai 2019((Mfalme wa Morocco Mohammed wa sita amewapa msamaha wafungwa 4,764 wakiwemo kadhaa waliokamatwa kuhusiana na maandamano ya kuipinga serikali mwaka 2016. Hatua hiyo ya mfalme inafuatia maadhimisho ya miaka 20 tangu alipotawazwa katika nafasi hiyo.
Msamaha wa mfalme wa Morocco kwa wafungwa ni agizo lililochapishwa jana usiku na shirika la habari la serikali la MAP likisema msamaha huo utawahusu pia wafungwa wanaokabiliwa na maradhi makubwa,pamoja na wale wenye ulemavu na waliofungwa kwa kesi zinazohusiana na ugaidi waliokamilisha mpango wa maridhiano.
Ikumbukwe mwaka 2016 wimbi la maandamano lilizuka katika mkoa wa kaskazini wa al Hoceima kupinga ukosefu mkubwa wa ajira na vitendo vya rushwa vilivyodaiwa kufanywa na serikali. Maandamano hayo yalifuatia kifo cha mchuuzi wa samaki aliyegongwa na lori la kubeba taka wakati akijaribu kuzuia samaki wake wasiharibiwe walipokuwa wakisombwa na maafisa polisi.
Hayo yalikuwa ni miongoni mwa maandamano makubwa kuwahi kutokea Morocco tangu mwaka 2011. Yaliiongozwa na kile kinachofahamika kama al Hirak al Shaabi au vuguvugu maarufu. Katika hotuba yake ya kuadhimisha miaka 20 ya mfalme Mohamed wa sita amezungumzia masuala mengi ikiwemo mageuzi.
''Tumechukua pia hatua muhimu za kuimarisha na kusisitiza haki na uhuru kwa ajili ya kuunga mkono mchakato imara na bora wa demokrasia. mbali na hayo tunafahamu kwamba licha ya mageuzi ya miundo mbinu na kitaasisi kuwa ni muhimu hayana athari kubwa''
Mfalme Mohammed wa sita ametowa pia mwito wa kufanyika mabadiliko serikali akitaka damu changa kuchukua uongozi akisema sera ya maendeleo ya taifa hilo haitoshi kufikia mahitaji ya wananchi. Mfalme huyo wa Morocco amesema kamati mpya itaundwa kusimamia utekelezaji wa mageuzi kadhaa katika sekta nyingi ikiwemo alimu,afya,kilimo na kodi.
Mwaka 2011 waandamanaji walioshawishiwa na wimbi kubwa la maandamano katika nchi nyingine za kiarabu walisababisha yafanyike mabadiliko ya katiba nchini Morocco na kulifanya bunge linalochaguliwa na wananchi kupewa mamlaka makubwa pamoja na waziri mkuu. Ingawa bado mfalme anabakia kuwa na mamlaka jumla kama kiongozi wa nchi ,amiri jeshi na mwenye mamlaka makubwa ya kidini katika nchi hiyo sambamba na kushikilia maamuzi kuhusu sekta muhimu za kiuchumi.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo