Mauaji ya mjini Jos, Nigeria
11 Machi 2010Maelfu ya wanawake waliovaa nguo nyeusi waliandamana mjini Jos wakiwa wamebeba misalaba ya mbao na picha za watoto waliouawa. Maandamano hayo yalitokea ikiwa ni siku ya kwanza ya mfungo wa siku tatu kwa madhumuni ya maombi ya kumuomba msamaha mwenyezi Mungu kufuatia mauaji katika jimbo la Plateau na kuombea amani na maridhiano kati ya Waislamu na Wakristo. Gavana wa jimbo la Jos, Jonah Jang alitoa wito wa kufanyika saumu hiyo ya siku tatu.
Na huku kukiwa bado taswira ya kuelekezeana kidole cha lawama kuhusu mauaji ya zaidi ya raia mia mbili viungani mwa mji wa Jos, wakaazi wanasema kwamba wataomba ili umwagaji damu usitishwe na kuwa hawana imani na walinda usalama.
Waandamanaji wengine walibeba Biblia na matawi ya miembe kama ishara ya umoja wakikariri kwamba hawawataki wanajeshi kwa sababu wameshindwa kudhibiti hali ya usalama.
Wanajeshi bado wanapiga doria katika mji wa Jos na viunga vyake ingawa wakaazi wanasema ni jitihada finyu na iliyochelewa. Mkaazi mmoja alisema wanaenda kanisani kulia kuhusu mauaji yaliyotokea.
Wanawake na watoto ndio walipata pigo kubwa zaidi katika mauaji hayo yaliyotekelezwa kwa saa tatu mapema siku ya Jumapili.
Idadi kamili ya waliofariki haijulikani na huku duru za polisi zikisema ni kiasi cha watu 109 waliofariki, kamishna wa mawasiliano katika eneo la mkasa anasisitiza kwamba ni kiasi cha watu 500 waliofariki. Hali ya wasiwasi bado imetanda kulingana na walioshuhudia kisa hicho cha mauaji.
Polisi imewakamata washukiwa 49 ambao ni wafugaji Waislamu kutoka kabila la Fulani kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji hayo ya Jumapili.
Nigeria ambayo ni nchi yenye idadi ya raia wengi zaidi barani Afrika, imegawanyika pande mbili za waislamu na wakristo.
Shirika la msalaba mwekundu limesema kiasi cha wakaazi 8000 wameyakambia makaazi yao. Kulingana na walioshuhudia, umati wa watu ulijaribu kulisimamisha lori waliloshuku lilikuwa limebeba wapiganaji na silaha. Maafisa wa polisi walipowasili waliwafyatulia risasi na wawili waliuawa na wengine watano walijeruhiwa. Amri ya kutotoka nje ilikuwa imetolewa katika jimbo la Jos.
Shirika la msalaba mwekundu linasambaza chakula cha msaada kwa takriban watu 5000 ambao wanapiga kambi katika vituo vya polisi.
Mwandishi, Peter Moss / AFP/ AP
Mhariri, Josephat Charo