Maelfu ya Wapalestina waondoka Gaza City
18 Septemba 2025
Mashambulizi makubwa katika jiji la Gaza yamepelekea maelfu ya watu kulazimika kuyahama makazi yao baada ya kuamriwa na jeshi la Israel. Msemaji wa Shirika la Kimataifa la kuwahudumia watoto UNICEF Tess Ingram ameiambia DW akiwa kusini mwa Gaza huko al Mawasi kuwa familia za Wapalestina zimeathiriwa na kuchoshwa na hatua hiyo ya kuhamishwa kila mara.
"Sheria ya kimataifa iko wazi. Watu lazima walindwe iwe wanaondoka au wameamua kubaki. Lakini kwa bahati mbaya, mara nyingi mno katika mzozo huu, tumeshuhudia sheria hizo za kimataifa zikipuuzwa, " aliongeza Tess Ingram.
Operesheni hiyo katika jiji la Gaza iliyoanza Jumanne na kuendelea Alhamisi, imeuchochea mzozo wa Mashariki ya Kati na kufifisha uwezekano wa kufikiwa mpango wa usitishaji mapigano. Jeshi la Israel ambalo limesema linalenga "kuharibu miundombinu ya kijeshi ya Hamas" halijaeleza shambulio hilo litadumu kwa muda gani lakini dalili zinaonyesha kuwa linaweza kuchukua miezi kadhaa.
Hayo yakiarifiwa, Kiongozi mkuu wa Hamas ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu shambulizi la wiki iliyopita la Israel huko Doha. Ghazi Hamad ameiambia Idhaa ya kiarabu ya Al Jazeera kwamba shambulio hilo lilifanyika wakati uongozi wa kisiasa wa Hamas ulipokuwa ukijadili pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano Gaza. Kiongozi huyo ameongeza kuwa walinusurika kwa "majaliwa ya Mungu" kutokana na shambulio hilo la kisaliti na kichokozi dhidi yao na Qatar.
Wakati huohuo, jamaa wa mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza walikusanyika jana usiku nje ya makazi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem huku wakitoa tuhuma kali dhidi yake. Ofir Braslavski, baba wa Rom Braslavski, ambaye pia ana uraia wa Ujerumani amesema alizungumza kwa njia ya simu na Netanyahu mwezi mmoja na nusu uliyopita na akamuahidi kumrejesha nyumbani kijana wake lakini sasa anafanya kinyume chake huku akiongeza kuwa mikono ya Netanyahu imejaa damu.
Maandamano yashuhudiwa pia Uhispania
Watu kadhaa walikusanyika kudhihirisha uungwaji wao mkono kwa Palestina na kulaani kinachoendelea huko Gaza. Miongoni mwa waandamanaji hao ni Manuela Carmena, meya wa zamani wa mji wa Madrid aliyekemea ukimya wa jumuiya ya kimataifa:
" Ukatili, mauaji ya watoto na ya watu wazima, ni mambo ya kutisha mno. Ni kana kwamba ghafla hakuna tena sheria, hakuna haki za binaadamu, kana kwamba ushetani umetuvaa.”
Wanasheria pia walijiunga na maandamano hayo yanayotazamiwa kuendelea hadi leo hii katika miji ya Madrid na Barcelona hasa yakifanyika mbele ya Balozi za Israel . Montserrat Abad ni Professa wa sheria ya kimataifa katika chuo kikuu cha Carlos III mjini Madrid ametoa wito wa hatua kuchukuliwa:
"Ni muhimu kukomesha hali ya kutochukua hatua, kwa sababu tunazungumzia uhalifu mkubwa zaidi ambao unaigusa jumuiya ya kimataifa kwa ujumla wake, nao ni: uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari."
Siku ya Jumatano, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza vikwazo kwa viongozi wa Israel na Hamas kufuatia mzozo unaoendelea huko Gaza huku Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV akikosoa hali mbaya ya kibinaadamu inayowakumba watu wa Palestina. Mamlaka za Gaza zimesema tangu kuanza kwa vita hivyo, sasa idadi ya vifo imefikia watu 75,000.
//AP, DPA, Reuters, AFP