Maelfu ya Wasyria wakwama
15 Aprili 2017Maelfu ya Wasyria wamekwama katika eneo la mji wa Aleppo kufuatia kusimamishwa makubaliano ya kuwahamisha watu kutoka vijiji vya Washia na kwa upande mwingine kuachiwa huru waasi wa Kisunni pamoja na familia zao kutoka miji ya karibu na Damascus. Hayo yameelezwa na wanaharakati wanaofuatilia hali ya vita vinavyoendelea Syria.
Shirika la kutetea haki za binadamu linalofuatia hali ya nchi hiyo lenye makao yake London Uingereza limesema tatizo limetokana na kutohakikishiwa usalama wa kuondoka waasi kutoka eneo la Zabadani mji ambao pia umejumuishwa katika makubaliano hayo. Makuabaliano hayo ni mojawapo ya mengine mengi yaliyofikiwa miezi ya hivi karibuni ambayo yametoa nafasi kwa serikali ya rais Bashar al Assad kuyadhibiti tena maeneo ambayo ilikuwa ikizingirwa na vikosi vyake kwa muda mrefu pamoja na washirika wake.
Katika makubaliano ya hivi karibuni mamia ya waasi na familia zao waliondoka mji wa Madaya karibu na Damascus na kusafirishwa kwa mabasi kuelekea mji unaodhibitiwa na vikosi vya serikali wa Aleppo.Kutokea hapo wanahitajika kusafirishwa kuelekea mkoa wa Idlib ambako ni ngome kuu ya waasi. Kadhalika kwa mujibu wa maafikiano,wapiganaji wanaoegemea upande wa serikali pamoja na wakaazi kutoka vijiji vinavyoshikiliwa na washia vya al-Faoua na Kefraya mkoani Idlib maeneo ambayo yote yamezingirwa na waasi waondokea na kupelekwa viunga vya mji wa Aleppo. Leo Jumamosi (15.04.2017) wale waotokea Madaya walikuwa wamekaa kwenye mabasi katika eneo linalodhibitiwa na serikali la Allepo wakisubiri kuondoka kuelekea Idlib na hayo yamethibitishwa kwa picha zilizotumwa na wanaharakati wa upinzani.
Wakati huohuo wakaazi kutoka vijiji vya Washia walikuwa pia bado wakisubiri katika maeneo yanayothibitiwa na waasi viungani mwa mji wa Aleppo kuingia katika mji huo wameeleza mashahidi. Wanaharakati wa upinzani wanasema kwamba waasi wamekuwa wakilalamikia hatua hiyo ya ucheleweshaji kwamba kwa kiwango fulani imesababishwa na ule ukweli kwamba idadi ndogo ya wapiganaji wa serikali wameshaondoka maeneo ya vijiji vilivyokamatwa na Washia kinyume na mambo yaliyovyotakiwa kufanyika. Kuna baadhi ya wakaazi katika kituo kimoja cha kufikia nje ya mji wa Aleppo ambako mabasi kutoka al-Foua na Kefyara yalikuwa yanasubiria wanasema kwamba hawana hakika wapi watakwenda kuishi.Katika mji huo wa Aleppo inasemekana kwamba watu wamekuwa wakisubiri hapo tangu Ijumaa usiku na hawakuruhusiwa kwenda kokote.
Hali inatisha kwa mujibu wa ripoti hakuna maji ya kunywa wala chakula.Na maeneo yalikoegeshwa mabasi yaliyowapakia watu hao ni maeneo madogo ambako mtu hawezi hata kupata nafasi ya kutoka na kuzunguka amesema kijana mmoja kwa jina Ahmed mwenye umri wa miaka 24.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Bruce Amani