1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya watoto watumikishwa kijeshi CAR

18 Desemba 2014

Shirika la hisani la Save the Children limesema maelfu ya watoto walikuwa wanatumika kama wanajeshi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita wakati wa vita vya kikabila na kidini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Afrika Zentralafrikanische Republik Kindersoldaten Resozialisierung
Picha: UNICEF/NYHQ2012-0881/Sokol

Nchi hiyo tajiri kwa dhahabu na almasi iliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kundi la waasi wengi Waislamu linalojiita Seleka kuipindua serikali ya rais mkristo Francois Bozize mwezi Machi mwaka 2013.

Kwa mujibu wa shirika la Save the Children, tangu wakati huo wavulana na wasichana elfu kumi waliuwawa, kubakwa na kuingizwa jeshini kama wapiganaji, vijakazi, wapelelezi na watumwa wa ngono.

Waasi wa kundi la Seeleka.Picha: picture alliance/AP Images

Wasimulia yaliyowakuta

Maeva ni miongoni mwa watoto hao na ana umri wa miaka 17, aliliambia shirika la Save the Children kuwa mwaka jana alijiunga na kundi la wanamgambo wa kikristo la Anti -balaka baada ya waasi wa seleka kumbaka na kumuua shangazi yake ambapo naye alijifunza kuua na kubainisha kuwa kuna wengine waliokuwa watoto wa miaka minane katika jeshi hilo .

Wanajeshi watoto wanakabiliwa na athari za kimaumbile na kiakili katika vurugu za wapiganaji na watu wazima ambapo wasichana mara nyingi wanatafuta ulinzi kwa kuwa wake wa wapiganaji huku wote wasichana na wavulana wana dhalilishwa kijinsia.

Grace Dieu alikuwa na umri wa miaka 15 alipoungana na mafunzo katika kundi la Seleka mwezi Disemba mwaka 2012 na anasema waliambiwa wasiwe ni watu wa kusamehe na huku wakijikuta kuwa watoto ndio wamewekwa mstari wa mbele wakati wa mapambano na kwa sababu wana kuwa wamevutishwa au kuleweshwa, hufanya jambo kama walivyoelekezwa.

Kwa upande wa Jean mwenye umri wa miaka 16, aliekuwa katika eneo la ukaguzi upande wa Seleka karibu na mji mkuu Bangui, aliliambia shirika la Save the Children kuwa alikuwa na bunduki aina ya AK47 ambayo alikiri kuuwa nayo watu wengi sana.

Wanamgambo wa Anti-Balaka.Picha: DW/Scholz/Kriesch

Akizungumza na watafiti, Jean alisema alikuwa anawaogopa sana viongozi wa kundi lake na pia alikuwa anawaogopa maadui wao wa kundi la Anti-balaka kama ilivyo kuwa inajulikana kuwa walikuwa wanakata vichwa kama walivyo wapiganaji wa Seleka na zaidi anarafiki zake ambao walikatwa vichwa.

Milioni 2.5 waathiriwa

Kwa upande wake, mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Watoto UNICEF ulisema kuwa angalau mtoto mmoja aliuwawa au alijeruhiwa kila siku mwaka huu huku watoto wawili kati ya watano wakihitaji msaada wa kibinadamu.

Takribani watoto milioni 2.5 wameathirika na mgogoro huu, na kwa mujibu wa UNICEF mamia wameuwawa au kujeruhiwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati . Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Afrika Magharibi na Kati Manuel Fontaine, watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hawapo tena kwenye vichwa vya habari, lakini zaidi ya watoto milioni 2.5 kati yao wanaendelea kuishi kwa wasiwasi.

Wanajeshi wa Ufaransa walioko Jamhuri ya Afrika ya Kati.Picha: Reuters/Siegfried Modola

Aidha shirika la hisani la Save the Children limabainisha, ukosefu wa fedha na ukosefu wa usalama ikiwa ni pamoja na vizuizi barabarani, uporaji ,na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada kumewaacha watoto bila ya upatikanaji wa huduma muhimu za afya, maji , elimu na ulinzi.

Takribani askari wa kulinda amani 2000 kutoka Ufaransa na 8000 kutoka Umoja wa Mataifa wameshindwa kuudhibiti mgogoro Jamhuri ya Afrika ya Kati nchi ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa tangu mwezi Disemba mwaka 2012. Maelfu ya watu wameuwawa na watu wapatao milioni hawana makaazi kwa sababau ya mgogoro huo.


Mwandishi :Zuhura Hussein/dpa.
Mhariri :Saumu Mwasimba.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW