1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kuripuliwa bwawa la Kakhovka: Maelfu ya watu hatarini

7 Juni 2023

Takriban watu 42,000 wako katika hatari ya kukumbwa na mafuriko kando na mto Dnipro baada ya bwawa la Kakhovka kuripuliwa hapo jana. Moscow na Kiev zimetupiana lawama ya kuhusika na uharibifu huo.

Ukraine Folgen Dammbruch Kachowka Staudamm
Picha: Planet Labs PBC/AP/picture alliance

Katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi wa Ukraine katika Umoja huo Sergiy Kylytsya ameishutumu Moscow kwa kulipua bwawa hilo na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na kusema kuwa ni kitendo cha ugaidi na mfano mwengine wa mauaji ya kimbari ya Urusi dhidi ya raia wa Ukraine.

Kwa upande wake  Balozi wa Urusi Vasily Nabenzya  amesema tukio hilo ni hujuma ya makusudi iliyofanywa na Ukraine na hilo linapaswa kuainishwa kama uhalifu wa kivita au kitendo cha ugaidi.

Wakati wa hotuba yake ya kila usiku, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema Urusi wamefanya uhalifu na uharibifu mkubwa wa ekolojia, si tu wakati huu wa vita bali kwa miongo kadhaa. Zelenskiy ameendelea kusema:

"Kwa hakika, Kakhovka ni mojawapo ya mabwawa makubwa nchini Ukraine. Miundombinu na hata kituo cha kuzalisha umeme cha Kakhovka vilikuwa chini ya udhibiti wa Urusi katika maeneo inayoyakalia kimabavu. Urusi walitega mabomu na kuripua bwawa hilo kwa makusudi ili kuulaghai Ulimwengu na kutumia mafuriko kama silaha."

Soma pia: Watu wahamishwa kufuatia shambulizi kusini mwa Ukraine

Washington imesema hadi sasa haikuwa na uhakika ni nani aliyehusika, lakini Naibu Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood amewaambia waandishi wa habari kuwa haiingii akilini kuwa Ukraine ingeliweza kuharibu bwawa hilo na kuwaathiri raia wake.

Maelfu ya watu hatarini

Mkazi wa eneo hilo akipita barabara iliyokumbwa na mafuriko baada ya kuta za bwawa la Kakhovka kuporomoka usiku kucha, huko Kherson, Ukraine.(Juni 6, 2023.)Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Mamia kwa maelfu ya watu wako hatarini kukumbwa na mafuriko na wamekuwa wakihamishwa kutoka kwenye makaazi yao, eneo la kusini la mto wa Dnipro nchini Ukraine. Maji mengi yanaendelea kutiririka kutoka bwawa hilo lililoripuliwa la Nova Kakhovka, na kuzifunika barabara na maeneo mengi ya mji huo.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya dharura na misaada ya kibinaadamu Martin Griffiths amesema uharibifu wa bwawa la kituo cha kuzalisha umeme cha Kakhovka ni mojawapo ya matukio  makubwa ya uharibifu wa miundombinu ya kiraia tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari, 2022.

Soma pia: Urusi yadai kuzima mashambulizi mengine ya Ukraine

Griffiths ameendelea kuwa matokeo rasmi ya janga hilo yatajulikana kikamilifu katika siku zijazo lakini akasema kuwa tayari madhara makubwa yanashuhudiwa kwa maelfu ya watu wa kusini mwa Ukraine ambao wamepoteza makazi yao, kukabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi na vifaa muhimu.

Wakati Ukraine ikijiandaa kwa mashambulizi yake makubwa ambayo yamekuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema mafuriko hayo yanaweza kuwa na faida kwa Urusi ili kupunguza kasi na uwezekano wowote wa vikosi vya Ukraine kupiga hatua muhimu eneo hilo.

(RTRE)