1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndia

Maelfu ya watu waandamana New Delhi dhidi ya Narendra Modi

31 Machi 2024

Maelfu ya watu wamehudhuria mkutano wa hadhara wa muungano wa vyama vya upinzani nchini India ambao umeikosoa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi kwa kuukandamiza upinzani kabla ya uchaguzi wa kitaifa.

Maandamano ya upinzani New Delhi
Wapinzani India wanadai Waziri Mkuu Modi anawakandamiza na kudhoofisha taasisi za demokrasia kabla ya uchaguziPicha: Manish Swarup/AP Photo/picture alliance

Maelfu ya watu wamehudhuria mkutano wa hadhara wa muungano wa vyama vya upinzani nchini India ambao umeikosoa serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi kwa kuukandamiza upinzani na kudhoofisha taasisi za kidemokrasia kabla ya uchaguzi wa kitaifa mwezi ujao. Mkutano huo uliopewa jina la "Okoa Demokrasia" ndio ishara ya kwanza kubwa ya hadharani ya muungano wa upinzani wa INDIA ya kupinga kukamatwa kwa afisa mwandamizi wa New Delhi aliyechaguliwa na kiongozi wa upinzani Arvind Kejriwal mnamo Machi 21.

Kejriwal alikamatwa na idara ya ujasusi wa kiuchumi, ambayo inadhibitiwa na serikali ya Modi, kwa tuhuma kuwa chama chake na mawaziri wadogo walikubali rushwa ya kiasi cha dola milioni 12 kutoka kwa wakandarasi wa kampuni za vileo karibu miaka miwili iliyopita.

Kukamatwa kwa Kejriwal kunaonekana kama pigo kwa muungano wa upinzani ambao ndio mpinzani mkuu wa chama cha Modi cha Bharatiya Janata - BJP, katika uchaguzi utakaoandaliwa kwa wiki sita kuanzia Aprili 19.

Viongozi wa upinzani wanakosoa kukamatwa kwa Kejriwal wakisema sio wa kidemokrasia na kukituhumu chama cha BJP kwa kulitumia shirika la serikali kuwadhoofisha, wakitaja mfululizo wa kamatakata na uchunguzi wa rushwa dhidi ya viongozi wakuu wa upinzani. BJP inakanusha kuulenga upinzani na kusema vyombo vya dola vinafanya kazi kwa uhuru.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW