Maelfu ya watu wapora vituo vya misaada Gaza, yasema UN
29 Oktoba 2023Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi na Misaada kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) limesema maelfu ya watu wamevunja maghala na vituo vya usambazaji wa misaada katika eneo la kati na kusini mwa Ukanda wa Gaza, na kuchukua vyakula na bidhaa nyingine muhimu.
Soma pia: Israel yatanua operesheni ya ardhini Ukanda wa Gaza
Thomas White, Mkurugenzi wa UNRWA amesema ishara hiyo inatia wasiwasi kwamba utaratibu wa kawaida wa kiraia utavurugwa baada ya wiki tatu za vita na mzingiro kwa Gaza na kuongeza kwamba watu wanahofu, wamechanganyikiwa na pia wamekata tamaa.
Hali ya usambazaji bidhaa Gaza ilikuwa mbaya hata kabla ya vita kuanza na imezidi kuvurugika kutokana na mzingiro na kusambaratika kwa watu. Takriban malori 80 yenye bidhaa yaliingia katika Ukanda wa Gaza kutoka Misri kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah tangu vita vilipozuka wiki tatu zilizopita.
Soma pia: UN yaonya kuwa watu wengi zaidi wataangamia Gaza
Jana Jumamosi hakuna msafara ulioweza kuingia Gaza kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya mawasiliano.
Mawasiliano yarejea taratibu Gaza
Hata hivyo, mawasiliano ya simu na intaneti katika mji wa Gaza, yaliyoharibiwa vibaya Ijumaa usiku wakati ndege za Israel zilidondosha mabomu na askari wake kuingia katika eneo hilo linalotawaliwa na Hamas, yanarejea taratibu leo Jumapili, vimeripoti vyombo vya habari vya Kipalestina.
Soma pia:UN: Israel na Hamas wanatenda uhalifu wa kivita
Kuvurugwa kwa mawasiliano kuliathiri operesheni za uokozi, huku watu waliokumbwa na mashambulizi ya angani wakishindwa kuomba msaada.
Wakati huo huo, Kanali Elad Goren wa Cogat, shirika la Wizara ya Ulinzi ya Israel linaloratibu na Wapalestina, amesema Israel itaruhusu ongezeko la misaada Gaza katika siku chache zijazo na raia wa Kipalestina wanapaswa kwenda katika kile kinachofahamika kama "eneo la kibinaadamu" kusini mwa Ukanda huo mdogo.
Jeshi la Israel laingia awamu ya pili ya operesheni Gaza
Jeshi la Israel limeyashambulia tena Jumapili maeneo kadhaa yalio chini ya udhibiti wa kundi la Hamas, huku likizidisha operesheni zake za ardhini katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi hilo limesema ndege za kivita ziliyapiga zaidi ya maeneo 450 ikiwa ni pamoja na vituo vya mawasiliano, uchunguzi, kutolea amri pamoja na vituo vya kurushia makombora. Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kwamba vikosi vyake vya wapiganaji vilishambulia pia vikundi vya kigaidi vilivyojaribu kujibu mashambulizi.
Kupitia mtandao wa X, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema, Israel inaingia katika awamu inayofuata ya vita vyake dhidi ya Hamas huko Gaza kuanzia mashambulizi ya angani, nchi kavu na baharini.
Wizara ya afya inayoongozwa na Hamas Gaza, imesema hadi sasa vifo vya watu ni takriban 7,326 tangu kuzuka kwa vita hivyo mnamo Oktoba 07.
Onyo la kuwahamisha watu hospitalini
Shirika la Hilal Nyekundu la Kipalestina limesema Jumapili kuwa limepokea onyo kutoka kwa maafisa wa Israel likilitaka kuwahamisha haraka watu kutoka hospitali ya al-Quds katika Ukanda wa Gaza. Limeongeza kusema kuwa mashambulizi yaliyofanywa Jumapili yalitokea umbali wa kilomita 50 tu kutoka hospitali hiyo.
Msemaji wa jeshi la Israel amekataa kuizungumzia taarifa hiyo. Maafisa wa Kipalestina wamesema karibu watu 50,000 wamepewa hifadhi katika hospitali ya Gaza Shifa na kusema wana wasiwasi kuhusu vitisho vinavyoendelea vya Israel kwenye hospitali hiyo.
reuters, dpa, ap, afp